Lissu aruhusiwa kutoka hospitalini

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu

Muktasari:

Ni baada ya miezi 11 akiwa wodini


Dar es Salaam. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ameruhusiwa kutoka hospitalini alipolazwa kuanzia leo ataishi nyumbani.

Tangu Septemba 7 mwaka jana aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 jijini Dodoma, Lissu amekuwa akiishi hospitalini kwa matibabu zaidi.

Ujumbe wa Lissu alioutoa leo Agosti 7, 2018 ameanza kwa kusema; “Hello Friends of Me!!! Good afternoon to y'all. Kwa mara nyingine nawaleteeni habari njema."

Amesema alfajiri ya Januari 6, 2018 aliondoka Hospitali ya Nairobi  nchini Kenya na kusafiri hadi Leuven nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu zaidi.

Lissu amesema jana Agosti 6, 2018 alitimiza miezi saba tangu alipowasili nchini humo.

“Leo Agosti 7 ni miezi 11 toka siku niliposhambuliwa na watu wanaojulikana sana kama 'watu wasiojulikana.'"

"Septemba 7 mwaka jana sikulala nyumbani kwangu. Agosti 7 ya leo, miezi 11 kamili baadae, nimeamkia nyumbani kwangu," amesema Lissu.

Ameongeza:  "Septemba 7 iliyopita wote mlikuwa na hofu kubwa kama ningemaliza siku hiyo au siku chache zilizofuata, nikiwa hai. Miezi 11 kamili baadae, Professor Dk Wilhelmus Jan Mertsemakers, daktari wangu tangu nilipokuja University Hospital Leuven, amesema sina sababu ya kitabibu ya kuendelea kukaa hospitali."

"Profesa Mertsemakers amesema nitaendelea na uponyaji nikiwa nyumbani kwangu. Nitatembelewa na  wauguzi kila siku nyumbani kuniangalia naendeleaje. Na nitarudi hospitali kumwona kila baada ya wiki mbili," amesema Lissu.

Katika ujumbe huo,  Lissu ameendelea kusema, bado ana chuma kubwa kwenye paja .

“Liko kama antenna ya TV za mwaka '47 na Profesa Mertsemakers amesema nitakaa nalo kwa si chini ya miezi sita. Lakini habari ya mujini ndio hiyo: nimetoka hospitalini."amesema.

Amemaliza kwa kusema:  "Hongereni sana kwa kazi nzuri ya kuniuguza na kuniponya na chochote mtakachokula au kunywa siku ya leo mnibakishie. Siko mbali."