Lissu ataja mchawi wa ugumu wa maisha

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu

Muktasari:

Makamu Wenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema ugumu wa maisha unaowakabili wananchi hivi sasa umesababishwa na Katiba iliyopo.

Dar es Salaam. Wakati malalamiko ya ugumu wa maisha yakiendelea kutamalaki nchini, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema kupanda kwa bei ya chakula na bidhaa mbalimbali kutakomeshwa kama Tanzania itapata Katiba mpya.

Lissu aliyerejea nchini leo, Januari 25, 2023 kutoka Ubelgiji alipokuwepo kwa miaka mitano, amesema licha ya kutokuwa na uwezo wa kushughulika upandaji wa gharama lakini hatakoma kulizungumzia.

Lissu ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Januari 25, 2023 jijini Dar es Salaam katika uwanja wa Bulyaga uliopo Temeke wakati wa mkutano wa hadhara wa kumpokea baada ya kurejea nchini akitokea Ubelgiji alikokuwa akiishi tangu mwaka 2018.

"Nataka nijitetee kwamba mimi sina mamlaka kisheria ya kupunguza bei hiyo, sina. Isipokuwa kuyazungumza tu... Kuyazungumza tu, hiyo nitaifanya haihitaji niwe na kacheo fulani," amesema.

Amesema ugumu wa maisha ni tatizo la kimsingi la kisiasa, kwani Mungu hajaamuru yote yanayofanyika bali ni mambo ya kibinadamu na kisiasa.

"Kwa sababu ni mambo ya kisiasa tuna mamlaka ya kuyaondoa, kwa hiyo kama umechoka kushindwa kununua maharage, sembe au tozo, hili liko ndani ya uwezo wetu, halihitaji maombi wala kumtishwa Mungu mambo yaliyopo kwenye uwezo wetu," amesema.

Ametoa kile alichokiita dawa ya matatizo hayo, kwamba itafutwe suluhu ya kisiasa itakayotokana na Katiba Mpya.

"Kwa wale wenye Katiba kuna kamstari mahali kwenye Katiba, kanakoelezea kwanini bei ya maharage ni sawa na bei ya nyama, Katiba inampa mamlaka makubwa Rais wa kuamua watu watozwe nini na kwa wakati gani" amesema.

Katika mkutano huo Lissu amesema Watanzania wanapaswa kuungana ili kudai Katiba mpya ili kuondoa matatizo yaliyopo hivi sasa.