Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu avuka kikwazo cha kwanza kesi ya rasilimali Chadema

Muktasari:

  • Lissu aliomba kuunganishwa katika kesi ya madai ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama na ubaguzi kati ya chama hicho upande wa Bara na wa Zanzibar. Wadai katika kesi hiyo walimwekea pingamizi, lakini leo ameshinda pingamizi hilo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amevuka kikwazo cha kwanza katika maombi yake ya kujumuishwa katika kesi ya madai ya mgawanyo usio sawa ndani ya chama hicho baina ya Bara na Zanzibar baada kushinda pingamizi.

Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

‎Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Lissu naye amewasilisha maombi, akiomba kuunganishwa kwenye kesi hiyo kama mdaawa mwenye masilahi.

Wajibu maombi katika shauri hilo ni pamoja na wadai katika kesi ya msingi yaani Said na wenzake  kwa upande mmoja na Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu ambao ni wadaiwa katika kesi ya msingi.

Hata hivyo wajibu maombi hayo ambao ni wadai katika kesi ya msingi, yaani Said na wenzake walimuwekea pingamizi la awali wakimpinga kuingia katika kesi hiyo, wakiiomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo ya Lissu bila kuyasikiliza.

Mahakama katika uamuzi wake leo, Jumanne, Machi 3, 2026, imelitupilia mbali pingamizi hilo baada ya kukataa hoja za wadai na kukubaliana na hoja za Lissu.

Katika pingamizi hilo ambalo lilisikilizwa Februari 17, 2026, wadai kupitia mawakili wao, Shaaban Marijani, Gido Simfukwe na Alvan Fidelis katika sababu ya kwanza walidai Lissu hajatimiza sifa za yeye binafsi kuingia katika shauri hilo.

Katika sababu ya pili walidai kwamba kiapo chake kinachounga mkono hati ya maombi hayo kina kasoro za kisheria kwa kuwa hajaweza kuthibitisha kuwa taarifa zilizomo amezipata wapi, kwani yuko gerezani tangu Aprili.

Lissu akijibu hoja hizo alidai kuwa ana masilahi stahiki kuingia katika kesi hiyo kwa mujibu wa Amri ya I, kanuni ya I - X (ya kwanza mpaka ya kumi) za Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Madai (CPC) zinaruhusu mtu mwenye masilahi katika shauri anaweza kuomba kuingizwa.

Akifafanua masilahi hayo, Lissu alisema yeye ni mwanachama wa Chadema tangu mwaka 2004 na kwa sasa ndiye mwenyekiti wa chama hicho, hivyo ana masilahi makubwa katika hiyo kesi kwa kuwa amri ambazo zitatolewa kama zilizoombwa zinamuhusu moja kwa moja kama mwanachama.

Kuhusu hoja ya uthibitisho wa taarifa zilizomo katika kiapo chake alikozipata wakati yuko gerezani amesema kuwa zinatokana na ufahamu wake binafsi.

Kwa mujibu wake yote yanayoendelea katika kesi hiyo anayafahamu kwa kuyasoma  tangu uamuzi wa Juni 10, 2025 wa zuio la chama kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi ya msingi itakapoisha.

Alisema kama upande wa wadai wana wasiwasi na ufahamu wake binafsi kuhusiana na taarifa hizo wanayo haki ya kumuita katika kizimba cha ushahidi na kumuhoji maswali ya dodoso kujiridhisha kama anadanganya au la.

Alipoulizwa na Jaji Mwanga kuwa amri hizo zikitolewa zinamgusa vipi alisisitiza kuwa yeye kama mwanachama amri yoyote inayotolewa kama ni kuzuia shughuli za chama au kama ni chama kudaiwa naye inamgusa moja kwa moja.

Kwa upande wake bodi ya wadhamini pamoja na Katibu Mkuu wa chama, kupitia kiongozi wa jopo la mawakili wake, Dk Rugemeleza Nshala, akishirikiana na Hekima Mwasipu waliunga mkono maombi na hoja za Lissu kuwa ana masilahi stahiki katika kesi hiyo.

Jaji Mwanga katika uamuzi wake leo pamoja na mambo mengine amesema kuwa baada ya kusikiliza hoja za pande zote anaona kuwa hoja za pingamizi hilo zinahitaji ushahidi  kuzithibitisha hivyo hazina mashiko kisheria.

Hivyo amesema kuwa hazistahili kuwa pingamizi la awali kwa kuwa linapaswa kuhusu mambo ya kisheria pekee na si ya kiushahidi.

"Kwa hiyo pingamizi hili linakataliwa," amesema Jaji Mwanga na kuongeza kuwa ni shauri hilo likasikilizwa na kutolewa uamuzi.

Kwa uamuzi huo sasa maombi hayo ya Lissu yanaingia katika hatua ya pili ambayo ni usikilizwaji ambapo mahakama itasikiliza hoja za msingi za mwombaji, kutaka kuunganishwa katika kesi hiyo na hoja ya wajibu maombi.

Baada ya hatua hiyo ndipo mahakama itatoa uamuzi wa ama kumkubalia Lissu kuunganishwa katika kesi hiyo au kumkatalia, kutegemeana na nguvu ya ushawishi wa hoja zake na hoja kinzani za wajibu maombi hayo.

Hivyo Jaji Mwanga sasa amepanga kusikiliza maombi hayo ya Lissu Machi 6, 2026.

‎Katika kesi ya msingi, wadai wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

‎Pia wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo wanaomba Mahakama hiyo itamke kuwa wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.

Pia wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa  ni kinyume cha sheria na ni batili.

Vilevile wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya Mahakama yatakapotekelezwa, na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na gharama za kesi.