Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu, Jamhuri sasa ni mwendo wa pingamizi

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, umemuweka njiapanda mshtakiwa huyo baada ya kumwekea pingamizi katika maombi yake ya kuutumia maelezo ya shahidi wao.

Hata hivyo, Lissu amejibu hoja hizo akieleza sababu ikiwemo kurejea kesi mbalimbali zilizopita na kuliomba jopo la majaji wanaosikiliza kesi yake kutokubali hoja za upande wa Jamhuri.

Lissu anakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, yenye shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, kwa lengo la kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchapisha maneno yafuatayo:-

"Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli... kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko... kwa hiyo tunakwenda kukinukisha. Sana sana huu uchaguzi tutakwenda kuuvuruga kwelikweli..., tunaenda kukinukisha vibaya sana..."

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, inaendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa Jamhuri.

Jana Oktoba 9, 2025 Mahakama hiyo ilianza kusikiliza ushahidi wa shahidi wa pili wa Jamhuri, ambaye ni Mkaguzi wa Polisi kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandaoni, Dawati la Doria Mtandaoni, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Makao Makuu, Dar es Salaam.

Shahidi huyo baada ya kuhitimisha ushahidi wake wa msingi, alioongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema, na leo Ijumaa, Oktoba 10, 2025, Lissu ameanza kumhoji shahidi huyo maswali ya dodoso kuhusiana na ushahidi wake huo alioutoa jana.

Baada ya kumhoji maswali machache, Lissu amesoma kwa sauti maelezo ya shahidi huyo kisha akaainisha maeneo 43 ambayo amesema yanakinzana na ushahidi wake alioutoa kwa mdomo.

Hivyo ameiomba mahakama iyapokee maelezo hayo yawe kielelezo cha upande wake, ili  ayatumie kuhoji kuaminika kwake kwa kuonesha mkinzano huo wa ushahidi alioutoa kwa mdomo akiwa kizimbani na kwa kiapo, na ule uliopo katika maelezo yake ya maandishi.

Katika ombi hilo Lissu ameirejesha mahakama hiyo katika uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika rufaa ya Lilian Jesus Fotes dhidi ya Jamhuri wa Septemba 2020 na Rufaa ya Shadrack Sospiter dhidi ya Jamhuri, uamuzi wa Machi 14, 2025, kuonesha kuwa amekidhi utaratibu uliowelwa na mahakama hiyo.


Pingamizi la Jamhuri

Ombi hilo la Lissu limepingwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Ajuaye Zegeli na Ignas Mwinuka wakidai kuwa mshtakiwa huyo hajafuata matakwa ya kisheria kuomba maelezo hayo ya shahidi wao huyo yapokewe kama kielelezo cha upande wake na ayatumie dhidi ya shahidi huyo.

Wakili Zegeli amesisitiza kuwa hata hizo kesi alizozirejea Lissu hajafuata zile taratibu zilizoainishwa.

"Sisi tunaona mshtakiwa ameshindwa kuielekeza mahakama hii vizuri kwa sababu bado hajam-cross examine (hajamdodosa) shahidi kwenye hayo maeneo ambayo ameyaainisha kwa mujibu wa hiyo kesi.

Kwa upande wake Wakili Mwinuka amedai kuwa  hawana shida na takwa la kwanza la mshtakiwa kusoma maelezo kwa shahidi, lakini matakwa mengine wanaona kuwa hayajatekelezwa.

Ameirejesha mahakama hiyo  katika uamuzi shauri la Jamhuri dhidi ya Mwanahawa Hamis maarufu kama Nyanda na wenzake tisa, shauri la uhujumu uchumi namba 2/2022, Mahakama Kuu, lililoamuliwa Oktoba 27, 2023 na Jaji Fredrick Manyanda.

Pia wakili Mwinuka amedai kuwa anayepaswa kutoa maelezo hayo kuwa kielelezo ni shahidi na si mshtakiwa na kwamba, hawajamsikia mshtakiwa akimuuliza shahidi kama anataka kuyatoa badala yake ni mshtakiwa mwenyewe tu ndio ameomba kuyatoa.


Majibu ya Lissu

Akijibu hoja hizo Lissu amedai kuwa utaratibu wa kuhoji uaminifu wa shahidi umewekwa na Mahakama ya Rufani kwenye shauri la Lilian Jesus Fotes (alilolirejea awali) na shauri la  Shadrack Sospiter dhidi ya Jamhuri, uamuzi wa Machi 14 2025.

Amedai kuwa msimamo wa kisheria na utaratibu huo hauwekwi na Mahakama Kuu bali unawekwa na Mahakama ya Rufani, na uamuzi wa kesi ya Mwanawala iliuorejewa na upande wa mashtaka hauwezi kutumika.

Amefafanua kuwa katika kesi ya Lilian Jesus Mahakama imesema, kwanza maelezo yasomwe, shahidi aelezwe kuwa maelezo yake yanakusudiwa kuhojiwa na kuoneshwa maeneo yenye mkinzano na tatu ni maelezo kupokewa.

Pia amedai kuwa alimuomba shahidi awasilishe maelezo yake labda kama mawakili wa Serikali hawakuwa makini kumsikiliza.

"Kwa hiyo waheshimiwa majaji nimefuata utaratibu, wameniletea huu uamuzi, siku ile nilikosea sikuwa nao lakini leo nifuata utaratibu. Hivyo, pingamizi hili halina msingi na naomba msilikubali," amehitimisha Lissu.

Hata hivyo, wakijibu hoja hizo za Lissu, Wakili Zegeli na Mwinuka wamedai kuwa bado msimamo wao ni kwamba utaratibu haujazingatiwa

Mahakama itatoa uamuzi wa pingamizi hilo  Jumatatu, Oktoba 13, 2025, kabla ya kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo.

Hii ni mara ya pili Lissu kuwasilisha ombi la namna hiyo akapingwa na Jamhuri. Awali, alifanya hivyo kwa shahidi wa kwanza lakini akawekewa pingamizi na baada ya kusikiliza hoja za Jamhuri alikiri kuwa kweli alilosea na Mahakama ikatupilia mbali ombi hilo