Lissu: Yakifanyika haya naweza kurejea Tanzania

Lissu: Yakifanyika haya naweza kurejea nchini

Muktasari:

  • Makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ameomba kuhakikishiwa mambo sita ili aweze kuanza safari ya kurejea nchini akitokea Ubelgiji anakoishi tangu Januari mwaka 2018.


Dar es Salaam. Makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ameomba kuhakikishiwa mambo sita ili aweze kuanza safari ya kurejea nchini akitokea Ubelgiji anakoishi tangu Januari mwaka 2018.

Lissu, aliyepelekwa kwa matibabu nchini Ubelgiji Januari 2018 baada ya kushambuliwa kwa risasi akitokea bungeni Dodoma Septemba 7, 2017, amelieleza Mwananchi kuwa mambo hayo yakifanyika, akirejea nchini ataishi kwa amani na hatakuwa na wasiwasi.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni kuhakikishiwa ulinzi na usalama wake, kusamehewa kwa wafungwa wote wa kisiasa, kupewa gari lake alilokuwa amepanda siku anashambuliwa kwa risasi, kulipwa gharama za matibabu, kupewa mafao yake ya ubunge na kesi zinazomkabili kuangaliwa kwa jicho la pili, akisema amebambikiwa.

Wakati Lissu akieleza hayo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema, “mara ya mwisho ilitolewa taarifa anasubiriwa Lissu aje achukuliwe maelezo yake ila alikataa, kwa maana hiyo uchunguzi haujakamilika. Mtu aliyetendewa kosa akikataa kuja polisi kuandika maelezo hawezi kukamatwa..., anatakiwa aje atoe maelezo yake.”
Mwananchi lilimtafuta Spika wa Bunge, Job Ndugai kuzungumzia suala hilo jana bila mafanikio, lakini mara kadhaa gazeti hili limewahi kumnukuu akisema Lissu alilipwa stahiki zake zote.

Lissu, aliyegombea urais kupitia Chadema katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka jana alisema aliporejea nchini na kushiriki uchaguzi huo alikuwa na walinzi, lakini baada ya uchaguzi waliondolewa, hali aliyodai ilitishia usalama wake.

“Nadhani mnakumbuka nilikamatwa nikapelekwa polisi baadaye nikaachiwa na jinsi nilivyoondoka huko, hili jambo na mengine nikihakikishiwa basi nitarejea,” alisema.

Lissu alimtaja Rais Samia Suluhu Hassan kuwa anaweza kumsaidia katika mambo hayo sita kwa sababu kiongozi huyo alipokuwa makamu wa Rais alikwenda kumjulia hali wakati amelazwa hospitali jijini Nairobi.

Baada ya kushambuliwa Dodoma, Lissu alipelekwa Nairobi, Kenya kwa matibabu kuanzia Septemba 8 mwaka 2017 hadi Januari 2018 na kati ya waliomtembelea ni Rais Samia wakati huo akiwa makamu wa rais, na kwenye mahojiano na gazeti hili makamu mwenyekiti huyo wa Chadema alisema kwa kitendo hicho ni wazi kuwa Samia anaweza kumsaidia.

“Nataka nielezwe waliotaka kuniua ni kina nani na nikirudi Tanzania nitakuwa salama kiasi gani.

“Je, nikirudi nitaendelea na kesi na nitakuwa huru kufanya siasa? Vipi kuhusu haki zangu walizokalia, hivi unajua sijalipwa na Bunge, hawakunilipa gratuity (kiinua mgongo),” alisema Lissu.

Akifafanua zaidi kuhusu haki zake bungeni, Lissu alisema alikuwa mbunge kwa miaka minne kuanzia mwaka 2015 kabla ya kuelezwa kuwa amepoteza sifa za kuwa mwakilishi wa wananchi Juni mwaka 2019, akisisitiza kuwa katika kipindi cha miaka hiyo minne hakupata kiinua mgongo.

“Pia wakati naugua sikulipwa gharama za matibabu na katika hili Rais Samia anajua nilikuwa wapi na alikuja kunijulia hali. Kimsingi hili nalo napaswa kupewa majibu ni kwa nini sikulipwa,” alisisitiza.

Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki mkoani Singida alihoji kuhusu lilipo gari lake alilokuwa amepanda siku anashambuliwa kwa risasi.

“Kwa nini wameshikilia gari langu wakati hakuna kesi wala uchunguzi wowote uliofanyika tangu niliposhambuliwa.

“Pia kama watawafungulia wafungwa wa kisiasa na kufuta kesi za kisiasa zinazowakabili wengi, nikiwemo mimi, kwa kweli nikipewa majibu ya haya ninarudi nyumbani,” alisema.
Kauli ya polisi

Akieleza zaidi kuhusu suala hilo, Misime alisema: “Kazi ya Jeshi la Polisi Tanzania kwa mujibu wa sheria za nchi ni kulinda maisha ya watu na mali zao. Kubaini, kuzuia kusimamia sheria na kudumisha amani na utengamano. Kulingana na mikakati iliyowekwa hali ya ulinzi na usalama ni amani na utulivu kwa wananchi, wakiwepo na wageni kutoka nchi mbalimbali.

“Hivyo kama kuna mtu anataka kuja

Tanzania, awe raia halali au mgeni anakaribishwa kwa sababu hali ya ulinzi na usalama ni shwari na ya amani kubwa,” alisema.

Misime alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi, Jeshi la Polisi hutoa ulinzi kwa wananchi wote bila ubaguzi na kama kuna mwenye changamoto za kiusalama ni jukumu lake kutoa taarifa kwa njia stahiki kwa mujibu wa sheria.

Msimamo wa Ndugai

Aprili mwaka jana, Spika Ndugai alisema Lissu amelipwa mishahara yake yote, ukiwamo wa Juni 2019 ambao anadai hajalipwa.

Alisisitiza kuwa amelipwa zaidi ya Sh200 milioni, posho mbalimbali zaidi ya Sh360 milioni na kwamba amelipwa zaidi ya Sh500 milioni kwa kipindi alichokuwa Ubelgiji. Alieleza hayo mara baada ya Bunge kupitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2020/2021.
Mbali na madai hayo, Spika alilitangazia Bunge kuwa Lissu alikuwa na madeni ya Sh70 milioni aliyokopa maeneo mbalimbali kupitia Bunge na kumtaka arejeshe fedha hizo.

Hata hivyo, alisema kama angeendelea, wangekwenda mbali zaidi na kuhoji jinsi alivyotumia fedha za wananchi, mishahara ya dereva wake na mafuta ya kumpeleka jimboni wakati akijua anazitumia isivyo halali kwa sababu yupo nje ya nchi, jambo ambalo lingemletea shida kwa kutakiwa kuzirudisha.
Nyongeza na Elias Msuya