Lori laanguka Kibaha, wananchi wakimbilia kuchota mafuta

Baadhi ya wananchi waliokutwa wakichota mafuta katika ajali ya lori eneo la Misugusugu, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, wakiondolewa eneo hilo na askari wa usalama barabarani.
Muktasari:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amewatahadharisha wananchi kukimbilia malori ya mafuta yanapopata ajali kwa sababu yanaweza kulipuka na kusababisha vifo
Morogoro. Lori la mafuta limepata ajali na kupinduka eneo la Misugusugu, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani huku baadhi ya wananchi wakifika kwenye tukio na kuanza kuchota mafuta yaliyokuwa yakivuja kwenye tenki la lori hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 14, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo leo huku akieleza hakuna madhara yaliyojitokea kwa binadamu.
Kamanda Lutumo amesema baada ya ajali hiyo kutokea, tenki zilizobeba mafuta aina ya petroli zilianza kuvuja, jambo lililosababisha wananchi wafike haraka eneo hilo na kuanza kukinga mafuta hayo.
“Ni kweli kuna ajali imetokea maeneo ya Misugusugu, Kibaha na baada ya kutokea kwa ajali hiyo, tenki zilianza kuvujisha mafuta aina ya petroli, wakati hilo likiendelea wananchi walifika na vibebeo mbalimbali na kuanza kukinga mafuta ili waondoke nayo, lakini baada ya kupata taarifa tulifika haraka na kuwadhibiti wananchi wote na tumewaondoa eneo hilo,” amesema Kamanda Lutumo.
“Hilo lori lilikuwa likifanya safari zake kutoka jijini Dar es Salaam kwenda mikoani na chanzo cha ajali ni kuacha njia na hadi sasa hakuna kifo, isipokuwa dereva amepata majeraha machache na anaendelea vizuri.”
Kamanda huyo amewatahadharisha wananchi kukimbilia malori ya mafuta yanapopata ajali kwa sababu yanaweza kulipuka na kusababisha maafa makubwa kwao ikiwamo vifo.
“Natoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kukimbilia magari yenye mafuta hasa petroli pale yanapopata ajali, maana ikitokea moto ukalipuka, yanaweza kutokea maafa makubwa, hivyo haifai ajali kama hizi watu kukimbilia na kuanza kuchota mafuta kama walivyofanya hawa wananchi wa Kibaha,” amesema.
Ajali hiyo inafanana na ile iliyotokea Agosti 10, 2019 katika eneo la Msamvu mjini Morogoro , watu zaidi ya 100 walipoteza maisha baada ya lori la mafuta lililopinduka kulipuka wakati wananchi wakichota mafuta.
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ilipokea majeruhi 47 waliofikishwa hospitalini hapo kwa nyakati tofauti wakitokea Morogoro ili kupatiwa matibabu na baadhi yao walipona na wengine kufariki dunia.