Lori lililobeba ufuta tani 32 laua dereva Lindi
Lori lililokuwa limebeba shehena ya ufuta kutoka Masasi mkoani Mtwara kuelekea Dar es Salaam likiwa limepata ajali katika eneo la Ingaula.
Muktasari:
- Ajali hiyo imetokea leo, Ijumaa Julai 3, 2026, saa 11 alfajiri, katika Barabara ya Dar es Salaam –Lindi, eneo la Daraja la Ingaula.
Lindi. Dereva wa lori lililokuwa limebeba tani 32 za ufuta amefariki dunia, huku watu wawili wakijeruhiwa baada ya lori hilo kupinduka katika Daraja la Ingaula, Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
Ajali hiyo imetokea leo, Ijumaa Julai 3, 2026, saa 11 alfajiri, katika Barabara ya Dar es Salaam –Lindi, eneo la Daraja la Ingaula.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Lindi leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori amesema lori hilo lilikuwa linatoka Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara kuelekea Dar es Salaam likiwa limebeba mzigo wa ufuta.
Amesema dereva wa lori hilo, aliyefahamika kwa jina moja la Pahala, mkazi wa Mtwara, amefariki dunia katika ajali hiyo, huku Oliva Gerald (31), utingo wa lori na Sikuzani Chama (42), aliyekuwa msindikizaji wa mzigo, wakijeruhiwa.
"Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Kinyonga, huku majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo," amesema Kamanda Imori.
Kwa mujibu wa Kamanda Imori, uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha ajali hiyo ni dereva kushindwa kulimudu lori alipofika kwenye kona, hali iliyosababisha gari hilo kupinduka.
Kutokana na tukio hilo, amewataka madereva na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuchukua tahadhari wanapokuwa safarini ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Fatuma Said, ameiambia Mwananchi kuwa alishuhudia tukio hilo alipokuwa akielekea shambani alfajiri.
"Nilikuwa napita eneo hilo kuelekea shambani ghafla nikaliona lori likiwa limeanguka darajani. Madereva wanapaswa kupumzika wanapohisi wamechoka badala ya kuendelea na safari na kuhatarisha maisha yao na ya wengine," amesema.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi limemkamata Mayunga Peter (32), mkazi wa Somanga wilayani Kilwa, kwa tuhuma za kuiba bajaji.
Kamanda Imori amesema mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa huku uchunguzi ukiendelea, na atafikishwa mahakamani mara utakapokamilika.