LSF yatoa ruzuku Sh3.1 bilioni kwa wadau wake
Muktasari:
- Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema, ruzuku hiyo inakwenda kuchochea pia utekelezaji mkakati wa kamapeni ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.
Dar es Salaam. Shirika la Legal Services Facility (LSF) limetoa ruzuku ya Sh3.1 bilioni kwa mashirika nufaika ya wasaidizi wa kisheria, mashirika simamizi kwenye kanda sita nchini.
Pia ruzuku hizo zinayahusu mashirika mengine yanayotekeleza miradi kwenye maeneo muhimu ya kijamii, hasa uchumi kwa ajili ya uwezeshaji kisheria kwa wananchi ikiwemo wanawake na watoto.
Taarifa iliyotolewa na LSF kwa vyombo vya habari leo Februari 23, imemnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng’wanakilala akisema, ruzuku hiyo inakwenda kuchochea pia utekelezaji mkakati wa kamapeni ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.
“Kampeni hiyo inajikita kutoa msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto kwa kutoa elimu katika jamii kuhusu haki za biandamu, kupambana na ukatili wa kijinsia.
“Pia itatoa utatuzi wa migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, kuelimisha wananchi kuhusu mifumo ya sheria, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala pamoja na kujenga uwezo miongoni mwa wadau wa sekta ya msaada ya kisheria nchini,” amesema.
Amesema sehemu ya ruzuku hiyo imetolewa kwa mashirika sita yatakayosimamia mashirika takribani 92 ya wasaidizi wa kisheria katika kanda sita nchini ili kuongeza ubora, uwezo, na maendeleo ya kitaasisi.
Ameongeza kuwa, ruzuku yenye thamani ya Sh2.08 bilioni imetolewa moja kwa moja kwa mashirika 184 ya watoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na wasaidizi wa kisheria nchi nzima Tanzania bara na Zanzibar.
Taarifa ya LSF imesema, sehemu ya ruzuku hiyo imetolewa kwa Shirika la Kilimanjaro Women Information Exchange and Community Organization (KWIECO) kwa ajili ya kutekeleza mradi kwenye eneo la utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ya usuluhishi.
“Mfumo wa utatuzi wa migogo kwa njia ya usuluhishi umeainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Ibara ya 107A (1) (d), ambayo inasisitiza kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro,” imesema taarifa hiyo.
Imesema, sehemu nyingine ya ruzuku imetolewa na LSF kwa mashirika matatu kwa ajili ya kutekeleza miradi katika maeneo maalumu ya kiuchumzikiwamo sekta za kilimo, madini, na uchumi wa bahari.
Mikoa itakayohusika ni pamoja na Manyara na Lindi kupitia taasisi tatu za Community Support Initiatives Tanzania (COSITA), Lindi Association of Non-Governmental Organizations (LANGO), na Civic Social Protection Foundation (CSP).
Eneo la mwisho la ruzuku hiyo ni mradi unaojulikana kama ‘Tanzanite Kwa Uchumi Imara wa Mwanamke’ utakaotekelezwa na LSF kwa kushirikiana na CSP, ukilenga kuboresha mazingira ya wanawake wajasiriamali kufanya biashara pamoja kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake kwenye mgodi wa Mirerani Mkoani Manyara.