Lukuvi amuweka ndani mkurugenzi kwa madai ya kuidanganya Serikali ya Tanzania
Muktasari:
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania, William Lukuvi amemuweka ndani mkurugenzi wa kampuni ya upimaji ya Geo Accuracy and Engineering, Watson Mwakalila kwa madai ya kuidanganya Serikali ya Tanzania.
Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania, William Lukuvi amemuweka ndani mkurugenzi wa kampuni ya upimaji ya Geo Accuracy and Engineering, Watson Mwakalila kwa madai ya kuidanganya Serikali ya Tanzania.
Amechukua uamuzi huo baada ya Watson kuzungumza uongo katika mkutano wa pamoja na kupeleka barua katika ofisi ya Serikali iliyokuwa na muhuri wa kampuni nyingine bila wahusika kuwa na taarifa.
Hayo yametokea leo Jumatatu Februari 24, 2020 katika mkutano wa Wizara ya Ardhi ulioshirikisha kampuni zinazofanya urasimishaji wa ardhi, wananchi walio na malalamiko na sekta za fedha
Akizungumza katika mkutano huo, Lukuvi amesema Mwakalila alikua akitoa maelezo ya uongo, “huyu ni mwongo sana kanidanganya tangu mwanzo, mwekeni ndani na akitoka asaini makubaliano ya lini atamaliza kazi hiyo na achukuliwe alama za vidole.
Katika kikao hicho, Watson alijikuta matatani baada ya kulalamikiwa na wananchi wa mtaa wa Mbezi Msakuzi kwa kushindwa kukamilisha kazi yake ya muda mrefu licha ya kupewa fedha.
Katika urasimishaji huo kampuni inayomilikiwa na Watson inazalisha viwanja 4,500 katika eneo la Msakuzi.
Katika utekelezaji wa kazi hiyo, Watson aliombwa na Manispaa ya Ubungo kuwasilisha kampuni ya upangaji atakayofanya nayo kazi ndipo aliitambulisha kampuni ya Apex Planning jambo ambalo lilimshangaza mmiliki wa kampuni hiyo.
“Hii kazi sijawahi kuisikia mimi, siyo kweli kwamba mimi ndiyo nachelewesha kazi hii, sina kazi yoyote ninayofanya naye. Kampuni yangu ni mpya imesajiliwa Julai 2019 na na muhuri tumepata Agosti na kazi ya kwanza tumefanya Tanga,” amesema Maggidi Bude, mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo.
Jambo hilo lilimkasirisha Lukuvi na kuagiza Watson awekwe ndani hadi kesho asubuhi Jumanne Februari 25, 2020, akitoka aseme atamaliza kazi hiyo lini.