Lungu apokonywa mafao ya kustaafu urais
Muktasari:
- Lungu alikuwa Rais wa Zambia kati ya mwaka 2015 na 2021, hata hivyo katika uchaguzi mkuu wa urais wa Agosti 12, 2021; alipoteza nafasi hiyo baada ya kushindwa na mpinzani wake na Hichilema, ambaye alipata zaidi ya kura milioni 2.8 (asilimia 59.4), dhidi ya milioni 1.8 (asilimia 38.3) za Lungu na kutangazwa mshindi.
Dar es Salaam. Waziri wa Habari na Mawasiliano Zambia, Cornelius Mweetwa amesema Serikali ya nchi hiyo imemwondolea mafao ya kustaafu, Rais wa zamani wa nchi hiyo Edgar Lungu, kwa kile kinachoelezwa amerudi kwenye ulingo wa siasa.
Waziri huyo ameyabainisha hayo jana Novemba 2, 2023; wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mji wa Kitwe, Kaskazini mwa nchi hiyo, huku akiirejea Sheria ya Mafao kwa Marais Wastaafu, ambayo kimsingi inazuia viongozi hao kushiriki siasa za vyama.
Mtandao wa TRT Afrika umemnukuu waziri huyo akisema: “...Kifungu cha 5 cha Sheria ya Marupurupu ya Marais Wastaafu, inaeleza mazingira ambayo viongozi hao wanaweza kuzuiwa mafao yao.”
Kwa mujibu wa Waziri Mweetwa, mojawapo ya mazingira hayo ni kurudi kwenye siasa, ingawa amesema kurejea kwa Rais huyo mstaafu (Lungu) katika ulingo huo, hakukitishii chama Tawala cha UPND ambacho kinaongozwa na Rais Hakainde Hichilema.
Waziri huyo amesema kuwa marais wastaafu hustahili mafao hayo pale ambapo wataonyesha kutofungamana na chama cha siasa.
Kama rais mstaafu nchini humo, Lungu alikuwa na haki ya kuwa na ulinzi wa maofisa wa usalama watatu, kumiliki pasipoti ya kidiplomasia, kupewa magari matatu ya serikali, nyumba iliyowekwa samani, bima ya matibabu na gharama za maziko baada ya kifo chake, pia sheria hiyo ilimpa kinga dhidi ya kufunguliwa mashtaka.
Hata hivyo imeelezwa kuwa Lungu bado hajazungumzia juu ya uamuzi huo wa Serikali.
Lungu alikuwa Rais wa Zambia kati ya mwaka 2015 na 2021, hata hivyo, katika uchaguzi mkuu wa urais wa Agosti 12, 2021; alipoteza nafasi hiyo baada ya kushindwa na mpinzani wake na Hichilema.
Hichilema mwenye umri wa miaka 61, ambaye alipata zaidi ya kura milioni 2.8 (asilimia 59.4) dhidi ya kura milioni 1.8 (asilimia 38.3) za Lungu, alitangazwa mshindi katika uchaguzi huo.
Lungu mwenye umri wa miaka 66, ambaye aligombea kwa kupitia Chama cha ‘Patriotic Front’ (FP), alikiri kushindwa na Hichilema na kuahidi kumkabidhi madaraka kwa amani.
Agosti 23, 2022, Lungu aliamua kustaafu siasa huku akisema: "Kwa makusudi kabisa nimeamua kuacha siasa ili watu wakubaliane na ukweli kwamba nimeamua kuanza maisha mengine; na sasa nahitaji kuwa mtumishi wa watu," amesema Lungu huku akionyesha kwamba atajitolea zaidi katika shughuli za kijamii.
Hata hiyo, zaidi ya mwaka mmoja baadaye (Oktoba 2023), mstaafu huyo alionyesha nia ya kurejea ulingoni.
Hii ni baada ya kunukuliwa akisema: "Mnaninataka nirejee kwenye siasa, mnataka nirejee? Nitafikiria," majibu hayo ya Lungu yalitokana na swali juu ya mwelekeo wake kisiasa wakati alipokuwa amemsindikiza mkewe Esther, aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka ya wizi katika mahakama moja mjini Lusaka.
Hata hivyo, Serikali iliwahi kumuonya mapema kuhusu kujihusisha kwake na siasa pale ilipomtuhumu kugeuza mazoezi yake ya kukimbia asubuhi kuwa mikutano ya kisiasa.
“...Kumekuwa na mikusanyiko isiyo halali na harakati za kisiasa zinazoendeshwa na makada wa chama cha FP wakati ambao Rais mstaafu Edgar Lungu alipokuwa akifanya mazoezi yake ya kukimbia asubuhi," Msemaji wa Polisi Rae Hamoonga amesema Septemba 25, 2023.
Akijibu juu ya hilo, Makebi Zulu ambaye ni wakili wa Lungu alisema: “Polisi lazima ijulishwe juu ya mikusanyiko ya watu,” hata hivyo, amesema kuwa rais huyo wa zamani hakuhitaji kibali cha polisi kufanya mazoezi ya ya kukimbia.
Zambia inatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwingine wa urais mwaka 2026.