Lusinde ashangaa Chadema kutumia rangi nyekundu kwenye bendera

Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde.

Muktasari:

Wananchi wa Ukonga, watapiga kura Jumapili ya Septemba 16, 2018 kumchagua mbunge wa jimbo hilo

Dar es Salaam. Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’ amekishangaa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutumia rangi nyekundu kwenye bendera ya chama akisema rangi hiyo haina uhalisia.

Akihutubia mkutano wa kampeni za ubunge wa Ukonga akimnadi Mwita Waitara, leo jioni Septemba 13, 2018 Lusinde amesema CCM inatumia rangi ya kijana kwa kuwa inaonyesha uhalisia wa mambo nchini.

"Mnawekaje bendera nyekundu, mlipigana vita wapi? Likipita gari la mzigo linaweka bendera nyekundu kwamba mzigo umezidi bodi sasa Chadema mzigo umezidi bodi vijana shukeni," amesema.

Lusinde amewataka wananchi wa Ukonga kuichagua CCM ili kutatua changamoto zao kwa kushirikiana na wabunge wa Chama hicho.

"Waitara shida za watu hautazimaliza zote wewe si Mungu. Utawasaidia kutatua changamoto shida zinamalizwa na Mungu," amesema.

Ameongeza "Watu wa Ukonga mnazo shida lakini vuteni subira. Tukifika bungeni tutasema wabunge wa CCM tumetumwa na Rais pelekeni umeme Ukonga," amesema.