Maalim Seif atoa ombi kwa viongozi wa upinzani Tanzania

Muktasari:

Mshauri mkuu wa ACT- Wazalendo, Maalim Seif atoa salamu za mwaka mpya chama hicho huku akiwataka viongozi wenzake wa upinzani kuondoa tofauti zao na kuwa kitu kitu kimoja ili kuiondoa CCM. Asema ataongoza juhudi za kuunda umoja wa dhati utakaoshirikisha vyama vya upinzani ili kukiondoa chama tawala.

Dar es Salaam. Mshauri Mkuu wa chama cha  ACT-Wazalendo nchini Tanzania, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka viongozi wenzake wa vyama vya siasa vya upinzani kuweka tofauti zao pembeni badala yake wawe  kitu kitu kimoja ili kuitoa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa makamu wa kwanza wa rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ametoa rai hiyo leo Jumanne Desemba 31,2019 wakati akitoa salamu za mwaka mpya wa 2020 za chama hicho kupitia mkutano wao na wanahabari akishirikiana na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe.

Amesema chama hicho kinautangaza mwaka 2020 kuwa ni mwaka kuiondoa CCM madarakani  huku yeye akijipa jukumu la kuongoza juhudi za kuunda umoja wa dhati utakaoshikisha vyama vingine vya upinzani, asasi za kiraia na vyama vya kitaaluma.

Katika mkutano huo, Maalim Seif amesema, “tutashirikisha makundi yote ya jamii na umoja huu utawaongoza wananchi kufanikisha lengo la kuiondoa CCM madarakani na kuleta mabadiliko mema nchini.”

“Nitoe wito kwa viongozi wenzangu wa vyama siasa pamoja na changamoto kadhaa zilizopo miongoni mwetu, bado maslahi yanatuunganisha kwa madhumuni ya kuing’oa CCM ni makamu kuliko tofauti zetu. Ni wakati wa kuziweka tofauti zetu pembeni na kuwaunganisha Watanzania pamoja kuiondoa CCM mwaka huu,” amesema Maalim Seif.

Amesema ACT- Wazalendo imejipanga kuwa 2020 ni mwaka ambao wananchi wanakwenda kuandika historia itakayoleta mabadiliko mema kwa Watanzania, akisema chama hicho kimejipanga kikamilifu kutekeleza wajibu na kuufikia mchakato huo.

Kuhusu mazingira ya Zanzibar, Maalim Seif amesema, “mmenidhulu Zanzibar katika chaguzi tano kuanzia mwaka 1995 hadi 2015. Uchaguzi wa 2015 ndio ulitia fora zaidi.

“Miaka yote nilifanya kazi ngumu ya kusimamia amani ya nchi na kuwatuliza Wazanzibari, lakini mwaka 2020 tutahakikisha tunazilinda kura,” amesema Maalim Seif.