Maaskofu wataka Watanzania kuwa wamoja, washtushwa kifo cha Rais Magufuli

Maaskofu wataka Watanzania kuwa wamoja, washtushwa kifo cha Rais Magufuli

Muktasari:

  • Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dk Fredrick Shoo ameeleza kupokea kwa mshtuko kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli na kuwataka Watanzania kuendelea kuwa wamoja.

Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dk Fredrick Shoo ameeleza kupokea kwa mshtuko kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli na kuwataka Watanzania kuendelea kuwa wamoja.

Dk Shoo ameyasema hayo leo Alhamisi Machi 18, 2021 wakati akitoa salamu za pole kuhusiana na kifo cha kiongozi huyo mkuu wa Kitaifa, kilichotokea jana Machi 17, 2021.

"Tumepokea kwa mshtuko, kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli, natoa pole kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu, familia ya Rais Magufuli, na Watanzania kwa ujumla,"

Vilevile Dk Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini amewataka Watanzania kuendelea kumuomba Mungu awape faraja katika kipindi hiki kigumu na kuliwezesha Taifa kusonga mbele.

"Niwaambie Watanzania, tuendelee kumuomba Mungu atupe faraja na kutuwezesha kuendelea mbele na tuendelee kudumisha umoja na mshkamano kama Taifa."

Kwa upande wake Askofu mstaafu wa kanisa la TAG, Mkoa wa Kilimanjaro, Askofu Glorious Shoo amesema Taifa limepata pigo kubwa kwa kumpoteza kiongozi mkubwa wa nchi na muhimu katika kipindi hiki na kwamba ataendelea kukumbukwa kwa mengi.

Shoo ambaye pia ni mchungaji kiongozi wa Kanisa la Kilimanjaro International Christian Center ameyesema hayo leo Alhamisi Machi 18, 2021 wakati akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu.

Amesema kipindi hiki ambacho Taifa limepoteza mtu muhimu ni vyema Watanzania wakachuja maneno ya kuzungumza  hasa katika kipindi hiki na kusema ni vyema jambo lolote likafanyika  kwa hekima na kwa uangalifu wa Kimungu.

"Taifa limepoteza baba ambaye ni mzito katika Taifa, kiongozi muhimu sana katika Taifa letu, tutaendelea kumkumbuka kwa mengi makubwa aliyoyafanya katika nchi hii,"amesema Askofu Shoo

"Jambo ambalo nawaombea Watanzania na viongozi wanaoendelea kuandaa mipango mbalimbali, mipango yote ifanyike kwa utulivu na kwa kumtumainia Mungun na ni kipindi ambacho cha kuepuka maneno yasiyokuwa la busara,"

"Ni muhimu sana kuchuja maneno yetu kipindi hiki ni kipindi ambacho hatupaswi kusema kwa haraka na kufanya kazi kwa haraka, tunapaswa kufanya kazi kwa hekima na kwa uangalifu wa Kimungu."

"Ombi langu kubwa kwa Taifa na viongozi waliosalia, maandiko yanasema "nguvu zetu zitakuwa katika kutulia na kutumaini "ndio maana nawaombea viongozi wetu kuendelea kufanya mipingo yote kwa utulivu na Amani," amesema Askofu Shoo

"Nawapa pole Watanzania wote tuendelee kuliombea Taifa hususani na viongozi wetu katika kipindi hiki,"amesema Askofu Shoo.