Mabadiliko ya kiutendaji yaibeba NiC kupata faida

Mkurugenzi Mtendaji wa NiC Insurance, Dk Elirehema Doriye.
Muktasari:
- Safari ya Shirika la Bima la Taifa (NiC), imegubikwa na milima na mabonde lukuki, huku likikumbana na hatari ya kuwa karibu kufutwa.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa NiC Insurance, Dk Elirehema Doriye amesema mikakati ya mabadiliko ya shirika hilo, ndiyo siri ya kuendelea kuwepo kwake
Amesema katika kipindi cha miaka 55 tangu kuanzishwa kwake, shirika hilo lilikuwa likipata hasara, hali iliyosababisha kutoonekana tija ya kuwepo kwake.
Dk Doriye ameeleza hayo jijini Dar es Salaam leo, Jumatatu Septemba 11, 2023 alipotoa taarifa ya mafanikio ya NiC katika kipindi cha mwaka 2019/2020-2021/22 kwa wahariri na waandishi wa habari.
Amesema hali mbaya ya shirika hilo nyuma ya mwaka 2019, ilisababishwa na uwepo wa watu wengi waliokuwa wanadai, ingawa baada ya uchambuzi baadhi yalionekana kuwa hewa.
Hali hiyo, kulingana na Dk Doriye ilisababisha haja ya kufanyika mabadiliko yaliyoanzia katika uongozi na ndiyo yaliyomuingiza katika nafasi hiyo ya ukurugenzi.
Mabadiliko ya uongozi, amesema yaliambatana na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
"Hii ilihusisha kuondoa maeneo yanayovujisha mapato au yanasababisha shirika lisipate faida," amesema.
Mabadiliko mengine, Dk Doriye amesema ni weledi wa kuhakikisha kila mfanyakazi anafanya shughuli zake kwa ubora na kuwa msingi wa mafanikio ya shirika.
"Tuliangalia kwa kiwango gani kila mfanyakazi atachangia maendeleo ya NiC, kuanzia mfanyakazi wa chini hadi wa juu kila mmoja tulihakikisha tunajua mchango wake ni nini," amesema.
Uwekezaji katika rasilimali watu ni mabadiliko mengine aliyosema yamefanyika kuhakikisha kunakuwa na wataalamu.
"Ili kupata tija, ililazimu kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye wafanyakazi, tuliongeza wafanyakazi kutoka taasisi nyingine Kati ya asilimia 25 hadi 30," amesema
Kulingana na Dk Doriye, mpango mkakati wa shirika hilo ilibadilisha kuliwezesha kufanya biashara badala ya kutoa huduma kama ilivyo kwa mengine mengi ya Serikali.
"Tulileta mabadiliko kwenye tafsiri ya utendaji kazi na nini na kwa namna gani tunavyopaswa kufanya, tulipitia upya, dira, dhima na misingi, zote tulizibadilisha ili ziendane na uhalisia wa biashara tunayofanya," amesema.
Amesema mpango mkakati wao uliakisi kuwa shirika hilo ni la kibiashara.
Mabadiliko hayo, amesema yalisababisha mtazamo mpya na ukaanza kujengwa kwa wafanyakazi ili watoe huduma kibiashara.
Maboresho mengine, amesema ni uwekezaji wa mifumo ya Tehama karibu asilimia 90, akisema kabla ya mwaka 1999 uendeshaji wa shughuli ulikuwa kwa karatasi.
"Tuliwekeza kuhakikisha tunapata taarifa sahihi za wateja na kuwapa huduma haraka, tulianzisha programu tumizi ya NiC kiganjani," amesema.
Uwekezaji huo, amesema uliongeza mapato ya shirika na hata kurahisisha huduma.
Mwaka 2019, amesema ulipaji wa madai ulichukua siku 35 hadi 45 lakini sasa ni siku saba, ikiwa ni matokeo ya mabadiliko.
"Ukiwasilisha madai yako na nyaraka tunakulipa ndani ya siku saba na zinaweza kupungua," amesema.
Miongoni mwa kazi ngumu katika safari hiyo, Dk Doriye amesema ni kurudisha imani ya wateja hali ambayo ilichagiza kubadilishwa kwa muonekano wa shirika.
Amesema maboresho hayo yameleta tija kwa shirika hilo, hadi kutambuliwa na kupewa chapa ya Superbrand Afrika Mashariki.
Tija nyingine zilizopatikana, amesema ni faida katika shirika hilo, akifafanua mwaka 2020 ni Sh33.6 bilioni, 2021 ni Sh63.5 bilioni na mwaka 2022 ni Sh63 bilioni.
"Kabla ya hapo shirika halikuwa linapata faida, lilikuwa moja ya mashirika yaliyokuwa katika hatihati ya kufutwa, kwa kuwa Serikali iliwekeza lakini haikupata tija yake," amesema.
Amesema kwa sasa NiC inatoa gawio na mwaka 2022 ilitoa Sh2 bilioni.
Kulingana na Dk Doriye, mabadiliko yaliyofanyika yamesababisha shirika hilo likue kwa asilimia 108, likimiliki soko kwa asilimia 16 hadi Desemba mwaka jana.