Mabadiliko ya tabianchi tishio Zanzibar

Muktasari:

  • Mabadiliko ya tabianchi yametajwa kuathiri mwenendo wa maisha hususani kwa wananchi wanaoishi katika ukanda wa pwani ambako kwa kiasi kikubwa athari za waziwazi zimebainika.

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuwa tishio visiwani humo kutokana na athari za moja kwa moja katika maisha ya wananchi.

 Othman ameyasema hayo leo Januari 25, 2023 ofisini kwake Migombani Zanzibar wakati akizungumza na Naibu Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Rick Shearn kuhusu masuala ya mazingira, ushirikiano, uchumi, jamii na maendeleo.

Amesema mabadiliko hayo yameathiri mwenendo wa maisha hususani wananchi wanaoishi katika ukanda wa pwani ambako kwa kiasi kikubwa athari za waziwazi zimebainika.

Ametaja viashiria vya athari hizo kuwa ni pamoja na maeneo mengi ya visiwa hivyo ya kilimo na makazi ya watu yamevamiwa na maji chumvi, hivyo kudhoofisha mavuno, kipato cha wananchi na hatimaye kuyumba kwa uchumi kuanzia mtu mmojammoja, familia na taifa.

“Bila shaka juhudi kubwa zinahitajika na ushirikiano wa pamoja ili kunusuru hali hiyo isiendelee, kwani inaathiri hata mipango ya Serikali kuwaletea wananchi maendeleo, ikiwemo utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu,” amesema Othman.

Ameeleza matumaini ya Zanzibar kupitia uhusiano mwema na mataifa mengine katika kukabiliana na athari hizo kwa haraka hasa wakati huu ambao mazingira ya kisiasa nchini yameanza kufunguka, sambamba na juhudi za kuendeleza maridhiano kufuatia uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Naye Balozi Shearn amesema nchi yake ipo tayari kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika utekelelezaji wa mikakati muhimu ya kukabiliana na tatizo hilo ili hali hiyo ambayo kwa sasa ni tatizo la ulimwengu, isiendelee kuleta athari zaidi.

Balozi huyo amesisitiza haja ya kuendelea na ujenzi wa demokrasia, utawala wa sheria na maridhiano ya kisiasa ili kuweka mazingira bora yatakayoleta fursa nyingi za maendeleo.