Mabaki ya mwili wa mwanamke aliyeliwa na mamba yapatikana

Wananchi wa Kata ya Chifunfu wakiwa kwenye doria ya kutafuta mabaki ya mwili ya mama aliyeliwa na mamba.

Muktasari:

  • Mabaki ya mwili wa mama aliyeliwa na mamba wakati akioga Ziwa Victoria akiwa na mumewe yamepatikana, huku wananchi wakiwa na simanzi kubwa juu ya tukio hilo.

Sengerema. Idara ya wanyamapori ikiongozwa na mkuu wa kitengo cha wanyamapori wilayani Sengerema, Paul Posian wakishirikiana na wananchi wamefanikiwa kupata mabaki ya mwili wa mwanamke aliyeliwa na mamba Februari 24, 2024 katika Kijiji cha Chifunfu kilichopo Sengerema mkoani Mwanza baada ya kufanya doria.

Mama huyo  aitwaye Chindula Bwile (34) amefariki dunia baada ya kushambuliwa na mamba aliyetokomea na mwili wake huku mumewe akishuhudia, alipokuwa akioga katika Ziwa Victoria saa 2 usiku.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Chifunfu, Denis Dominic amesema mabaki ya mwili wa mama huyo yamepatikana kwenye  mapango ya mawe  yaliyoko ndani ya Ziwa Victoria, huku viungo mbalimbali vikiwa vimeliwa na mnyama huyo.

Posian amesema baada ya kuupata mwili huo, bado wanaendelea na  msako wa mamba hao ambao wanaonekana kuwa tishio, huku akitoa pongezi kwa wananchi kwa ushirikiano wao uliofanikisha kupatikana kwa mwili huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa idara ya wanyamapori ili wafanikishe kuwavuna mamba hao.

Nyandele Ernest ambaye ni mume wa marehemu, amewashukuru wananchi kwa kutoa ushirikiano ambao umefanikisha kupata mabaki ya mwili wa mke wake.

Marehemu Chindula Bwire ameacha mume na watoto watatu .