Mabala ataka ubia wa elimu sekta binafsi, umma

Muktasari:

  • Mdau wa elimu, Richard Mabala ameshauri kuwepo kwa ubia wa elimu kati ya sekta binafsi na sekta ya umma ili watu wengi wachangie kwa kuandika vitabu ambavyo vitapitishwa na kuratibiwa na Taasisi ya Elimu na sio taasisi hiyo kubeba jukumu la kuandika vitabu vyote.

Dar es Salaam. Mdau wa elimu, Richard Mabala amesema ni muhimu kuwa na ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma katika kuandika vitabu vya elimu badala ya kuliacha jukumu hilo kwa Taasisi ya Elimu (TET) pekee.

Mabala ameyasema hayo leo Mei 17, 2023 wakati akichokoza mada kwenye mjadala wa Mwananchi Twitter Space uliokuwa ukijadili rasimu ya sera ya elimu na mitalaa ambayo bado inajadiliwa.

Amesema sekta ya elimu inatakiwa kuhusisha wadau mbalimbali ambao watachangia vitu tofauti vitakavyosaidia kuboresha elimu hapa nchini.

“Ni muhimu kuwa na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuandaa vitabu vya kiada na ziada. Tufungue huu mlango ili watu wengi waweze kuchangia elimu kwa kuandika vitabu ambavyo vitapitishwa na kuratibiwa na Taasisi ya Elimu na sio taasisi hiyo kubeba jukumu la kuandika vitabu vyote,” amesema Mabala.

Mabala amesema angependa kuona wanafunzi wakifundishwa kuwa tayari kupokea mabadiliko yatakayotokea kabla hata hawajajua ni mabadiliko gani.

“Inabidi tuwafundishe watoto wetu wawe tayari kupokea mabadiliko bila kujali mabadiliko gani yatatokea. Tunapoongela kuajirika tusiongelee tu stadi za kazi huku tukisahau stadi 21.

“Binafsi bado ningependa kuona stadi za maisha ingekuwa somo linaloonekana, sera inataja lakini haionyeshi zinaingia wapi. Walimu wangepewa kozi maalum ya stadi za maisha,” amesema Mabala.

Awali akizungumza katika mjadala huo, mwandishi wa habari za elimu wa gazeti la The Citizen, Jacob Mosenda amesema anatamani mfumo wa elimu nchini ubadilike ili uendanane na wakati pamoja na teknolojia.

Amesema mchakato huo sio lelemama kwani umechukua rasilimali fedha na muda kuufanikisha. Amesema ni mafanikio makubwa kufikia hatua hii ambayo rasimu hiyo imefikia leo.

“Nilitamani kuona elimu inabadilika, kuona vitu mbalimbali katika sera na mfumo mzima wa elimu unabadilika na kuendana na wakati wa sasa. Kwa namna teknolojia inavyokuwa na uwanda wa ajira unavyozidi kuongezeka ni dhahiri tunahitaji mabadiliko,” amesema.

Mosenda amesema Serikali ione haja ya kuwa na lugha ya kufundishia na kama lugha itakuwa Kiingereza basi ifundishwe kuanzia ngazi ya chini kabisa na ikiwa ni Kiswahili basi kifundishwe kwa umahiri ili kuondoa mkanganyiko.

“Uamuzi wa Serikali kupanua wigo wa lugha za kufundishia kama Kifaransa, Kichina na Kiarabu ni mzuri kwa kuwa tayari kuna shule zilikuwa zinafundisha kwa lugha hizi ila sasa itaenda kuratibiwa na sera,” amesema.

Ameongeza kwamba: “Ninachokiamini sera hii ni muhimu na rasimu tumeisubiri kwa muda mrefu, tunategemea Serikali inakwenda kuitekeleza.”