Mabilioni yatengwa kusambaza maji Same na Mwanga

Muktasari:

Zaidi ya Sh3.7 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kusambaza maji katika vijiji 12 vya Wilaya ya Mwanga na Same ambavyo havina huduma ya maji safi na salama tangu kuanzishwa kwake.

Moshi. Zaidi ya Sh3.7 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kusambaza maji katika vijiji 12 vya Wilaya ya Mwanga na Same ambavyo havina huduma ya maji safi na salama tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza leo Jumatatu Machi 8, 2022 meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) mkoani Kilimanjaro, Weransari  Munis amesema  wameendelea kuweka  katika bajeti  vijiji ambayo havina huduma ya maji kabisa

Amesema wamejiwekea mikakati  ya miaka mitatu kuhakikisha  wanaweka  maji katika vijiji 32 ambavyo havijawahi kuwa na maji na kwa mwaka 2020/21, vijiji 12 vya wilaya ya Mwanga na Same vitapata maji.

Amebainisha kuwa wilayani Same kuna vijiji 14 ambavyo havina huduma ya maji na 18 kwa  Wilaya ya Mwanga, “ yapo maeneo mengine ambayo  tayari yalishakuwa na miradi ya maji  lakini kunahitaji uboreshaji.”

"Vijiji 12 vilivyo na wakazi  26,232 Wilaya ya Mwanga na Same vimewekewa makadirio ya bajeti ya zaidi ya Sh3.7 bilioni kwa ajili ya kusambaziwa maji katika mwaka wa fedha 2021/22.”

Amebainisha kuwa mwaka wa fedha 2020/21 kupitia Ruwasa mkoa  umetengewa Sh6.9 bilioni zitakazotumika katika kukarabati na kupanua miradi ya maji iliyopo.

Mbunge wa Moshi vijijini,  Professa Patrick Ndekidemi aliwataka  Ruwasa kuhakikisha wanasambaza maji safi  katika maeneo ya shule  kwa kuwa nyingi hazina maji safi na salama.