Mabomu ya machozi yalimtoa mafichoni

Muktasari:
- Taarifa mpya za mashuhuda wa tukio la shambulizi la risasi lililoua watu askari watatu wa polisi, mmoja wa kampuni na kujeruhi askari wengine sita, zimeendelea kuibuka, zikiwemo zinazobainisha jinsi mabomu ya machozi yalivyomkurupua muuaji na polisi wakapata fursa ya kummaliza.
Dar es Salaam. Taarifa mpya za mashuhuda wa tukio la shambulizi la risasi lililoua watu askari watatu wa polisi, mmoja wa kampuni na kujeruhi askari wengine sita, zimeendelea kuibuka, zikiwemo zinazobainisha jinsi mabomu ya machozi yalivyomkurupua muuaji na polisi wakapata fursa ya kummaliza.
Mmoja wa mashuhuda Mende Ebeneza ambaye ni mfanyakazi katika ofisi za Bodi ya Utalii zilizopo katika eneo hilo, alisema wakati mtu huyo aliyetambulika kama Hamza Mohammed amejibanza katika kibanda cha Ubalozi wa Ufaransa, polisi walimtupia mabomu mawili ya machozi akalazimika kutoka.
Akisimulia kisa hicho, shuhuda huyo alisema, “tulianza kusikia milio ya risasi ikitokea upande daraja la Selander na sekunde kadhaa nilipotoka nje nikaona watu wanakimbiakimbia, sikuelewa tatizo nini, nikadhani majambazi wamevamia. Alisema baada ya dakika kama ishirini wakawa wanasikia risasi zinasogea upande wa pili wa barabara.
“Tukamuona huyo mhusika, mimi niliripoti kwa mtu mmoja wa usalama kuwa eneo nilipo kuna hali si salama tunasikia milio ya risasi inarindima.
Soma zaidi: Familia inayodaiwa ya muuaji yasombwa na polisi
“Dakika kadhaa askari wakaja na gari mbili, wakaingilia geti letu wakaanza kutambaa na ukuta, hivyo wakawa na uwezo wa kumuona mhusika na kuanza mashambulizi.
“Kwa namna nilivyoshuhudia, polisi walijitahidi lakani jamaa alikuwa vizuri sana kwa mashambulizi, kwa dakika 20 hadi 25 kulikuwa na majibizano ya risasi.
Bomu la machozi
Baada ya hapo kuna bomu la machozi lilitupwa pale kwenye kibanda cha walinzi wa ubalozi ambako alikuwa amejificha yule jamaa, akitoka na kurusha risasi. Polisi wakatuma bomu la machozi lingine, likamtoa kwenye kile kibanda,
“Hapo nadhani alikosa hewa akatoka anayumba kurudi barabarani. Hapo ndio askari wakapata nafasi ya kumpiga na Shuhuda huyo alisema kuna haja ya mafunzo ya namna ya kujihami kwa wananchi yanapotokea mazingira kama hayo kwa kuwa endapo mhusika angekuwa na nia ya kudhuru wananchi wote mbele yake, angewadhuru wengi sana lakini hakuwa na haja na watu wa kawaida.
Soma zaidi: Wafanyakazi wa Hamza mgodini wamzungumzia
Kiukweli hapa sisi ofisi tulikuwa kila mtu anatafuta njia yake, kukitulia tunaendelea na kazi lakini tukisikia tena milio ya risasi kila mtu anakimbia kujificha. Hadi huku katika eneo letu tumeshuhudia maganda ya risasi lakini pia ukuta umetobolewa kwa risasi.
Tukio hilo lilitokea katika makutano ya Barabara ya Kenyata, Kinondoni na Ali Hassan Mwinyi sehemu maarufu kwa wafanyabiashara na makazi ya watu.
Jana shughuli katika eneo hilo zilikuwa zinaendelea kama kawaida. Katika eneo ambalo tukio lilitokea juzi kulikuwa na askari wawili wenye silaha, mmoja ndani ya banda na wengine akiwa amesimama mita takribani 10 kutoka lilipo banda hilo. Mfanyabiashara katika eneo la Selander, Tarick Abeid alisema “ni tukio linaloogopesha sana lakini hatuna jinsi tumeamua tu turudi kuendelea na biashara zetu kujiongezea kipato.”