Familia inayodaiwa ya muuaji yasombwa na polisi

Familia inayodaiwa ya muuaji yasombwa na polisi

Muktasari:

  • Familia inayodaiwa ni ya mtu aliyekuwa akipambana na polisi imechukuliwa na jeshi hilo jana usiku kwa ajili ya mahojiano zaidi.


Dar es Salaam. Familia inayodaiwa ni ya mtu aliyekuwa akipambana na polisi imechukuliwa na jeshi hilo jana usiku kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Jana, Jumatano Agosti 25, 2021 usiku, polisi walifika katika nyumba iliyotajwa alikuwa akiishi mtu aliyewaua askari wanne, akiwamo mmoja wa kampuni ya ulinzi.

Gazeti la Mwananchi liliweka kambi eneo hilo lililopo Upanga Mtaa wa Fire, Dar es Salaam.

Awali, kabla ya kuichukua familia hiyo, polisi walikuwa wameiweka chini ya ulinzi nyumba inayoelezwa alikuwa akiishi mtu huyo.

Wakiwa kwenye nyumba hiyo, polisi waliongozana na mwenyekiti  wa Serikali ya mtaa huo na kuingia ndani kwa kile kilichodaiwa ni kuzungumza na familia ya muuaji huyo.

Polisi, walipoulizwa kinachoendelea kwenye nyumba hiyo, walidai uchunguzi bado unaendelea na watatoa taarifa baada ya kukamilisha.

Mtu huyo ambaye pia aliuawa kwa risasi, jana alizua taharuki maeneo ya makutano ya barabara za Kinondoni na Kenyatta baada ya kufyatua hewani risasi huku akisikika kuwa anawatafuta polisi.