VIDEO: Askari watatu wauawa tukio la kurushiana risasi Dar

Askari watatu wauawa tukio la kurushiana risasi Dar

Muktasari:

  •  Watu wanne wamefariki dunia na sita kujeruhiwa kwenye mapambano ya kurushiana risasi yaliyotokea makutano ya barabara ya Kenyatta na Kinondoni jirani na Ubalozi wa Ufaransa, jijini Dar es Salaam.

  


Dar es Salaam. Watu wanne wamefariki dunia na sita kujeruhiwa kwenye mapambano ya kurushiana risasi yaliyotokea makutano ya barabara ya Kenyatta na Kinondoni jirani na Ubalozi wa Ufaransa, jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano Agosti 25, 2021 baada ya mtu mmoja ambaye hajafahamika kuzua taharuki baada ya kufyatua hewani risasi huku akisikika akisema kuwa anawatafuta polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo , Mkuu wa Operesheni Maalumu Jeshi la Polisi, CP Liberatus Sabas amesema kati ya watu wanne waliofariki dunia watatu ni askari polisi, huku mmoja akiwa mtumishi wa Kampuni ya Ulinzi ya SGA.

“Tumekutwa na tukio moja baya kabisa la kihalifu ambalo limepoteza maisha ya watu wanne na watatu kati yao wakiwa ni askari polisi, tukio hilo limetokea katika makutano ya barabara ya Kenyatta na Kinondoni, askari wetu walikuwa kazini,” amesema.

“Wakiwa kazini alikuja mtu mmoja akawashambulia askari hao kwa silaha ya aina ya bastola baada ya kuwashambulia na kuanguka alichukua bunduki zao mbili na kuanza kurusha risasi ovyo na kuelekea ubalozi wa Ufaransa alivyofika eneo la ubalozi wa Ufaransa kwenye kibanda akawa anajihamia kwenye kibanda huku akifyatua risasi ovyo.”

Ameeleza kuwa wanaendelea kufuatilia na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa…