IGP Sirro: Askari wawili wameuawa tukio la kurushiana risasi Dar

Muktasari:

  • Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, (IGP) Simon Sirro amethibitisha kuuawa kwa askari wawili kwenye mapambano ya kurushiana risasi yaliyotokea eneo la Daraja la Salenda jirani na Ubalozi wa Ufaransa, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, (IGP) Simon Sirro amethibitisha kuuawa kwa askari wawili kwenye mapambano ya kurushiana risasi yaliyotokea eneo la Daraja la Salenda jirani na Ubalozi wa Ufaransa, Dar es Salaam.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano Agosti 25, 2021 baada ya mtu mmoja ambaye hajafahamika kuzua taharuki baada ya kufyatua hewani risasi huku akisikika akisema kuwa anawatafuta polisi.

Akizungumza katika kikao kazi cha maofisa wa polisi, Sirro amesema mtu huyo naye ameuawa kwa kupigwa risasi.

“Mmeziona clip zinaruka sasa hivi akaingia barabara kubwa akawa anatamba na SMG na yeye amepigwa risasi na askari wetu hivyo, askari wetu wamefariki na yeye amefariki” amesema IGP Sirro.

Ameeleza kuwa wanaendelea kufuatilia kufahamu mtu huyo ametokea wapi na baadaye watatoa taarifa kamili.

IGP Sirro amenukuliwa kupitia kipande cha video kilichorushwa kwenye mtandao wa kijamii wa Wasafi Fm.