Wafanyakazi wa Hamza mgodini wamzungumzia

Wafanyakazi wa Hamza mgodini wamzungumzia

Muktasari:

  • Wananchi wa Kitongoji cha Kitete, Mamlaka ya mji mdogo Makongolosi wilayani Chunya wameeleza masikitiko yao kufuatia kifo cha Hamza Hassan Mohamed aliyeuawa na polisi jijini Dar es Salaam Jumatano Agosti 25, 2021.


  

Chunya.Wananchi wa Kitongoji cha Kitete, Mamlaka ya mji mdogo Makongolosi wilayani Chunya wameeleza masikitiko yao kufuatia kifo cha Hamza Hassan Mohamed aliyeuawa na polisi jijini Dar es Salaam Jumatano Agosti 25, 2021.

Hamza aliyekuwa akifanya biashara ya madini alifikwa na umauti baada ya kupigwa risasi na polisi dakika chache tangu alipofanya mauaji ya askari polisi watatu na mlinzi wa kampuni binafsi karibu na ubalozi wa Ufaransa na daraja la Salenda.

Wakizungumza na Mwananchi Digital baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Kitete wamemwelezea kwa namna tofauti kuwa alikuwa akiishi maisha ya kawaida,  kwamba  licha ya kuwa na migodi katika kitongoji hicho  hakuwahi kujikweza na  alishiriki shughuli zote za maendeleo kama wananchi wengine.

William Heneriko amesema, "niliishi naye kama rafiki kwa kweli na katika mgodi wake aliniajiri kama kiongozi wa mgodi wake. Nimefanya naye kazi sana na mwisho ilikuwa Juni mwaka huu."

Mohamed Hussein ni mmoja wa vijana waliokuwa wakiishi na Hamza anabainisha kuwa alimuita kaka na alikuwa akimshauri katika kazi walizokuwa wanafanya.