VIDEO: Majirani wamzungumzia kijana anayedaiwa kufanya mauaji Dar

Familia inayodaiwa ya muuaji yasombwa na polisi

Muktasari:

  • Ilikuwa ni mshike mshike katika makutano ya barabara ya Kinondoni, Kenyatta na Ali Hassan Mwinyi jana Jumatano Agosti 25, 2021, baada ya mtu mmoja ambaye hajafahamika kuwaua askari wanne, wakiwamo watatu wa Jeshi la Polisi na mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi.

Dar es Salaam. Ilikuwa ni mshike mshike katika makutano ya barabara ya Kinondoni, Kenyatta na Ali Hassan Mwinyi jana Jumatano Agosti 25, 2021, baada ya mtu mmoja ambaye hajafahamika kuwaua askari wanne, wakiwamo watatu wa Jeshi la Polisi na mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi.

Mtu huyo aliyedaiwa kushuka katika gari aina ya Toyota Noah, alianza shambulizi lake kwa kuwaua askari polisi wawili waliokuwa kwenye kibanda cha kupumzikia kilichopo makutano ya barabara hizo.

Baada ya kuwaua kwa kutumia bastola yake, alichukua bunduki mbili walizokuwa nazo na kuanza kurusha risasi hovyo na baadaye kukabiliana na askari wa Jeshi la Polisi waliofika eneo hilo.

Hali hiyo ilisababisha taharuki kwa watumiaji wa barabara hiyo kukimbia hovyo na wengine kulazimika kuacha vyombo vyao vya usafiri. Katika mapambano hayo mtu huyo alipoteza maisha kwa kupigwa risasi akiwa mbele ya lango la Ubalozi wa Ufaransa baada ya mapambano makali.

Katika kuhakikisha usalama kwenye eneo hilo, Polisi wadhibiti kwa kufunga barabara zote jambo lililosababisha msongamano wa magari.

Kauli za majirani kuhusu muuaji

Mara baada ya tukio hilo, taarifa mbalimbali zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa, muuaji huyo ni mkazi wa Upanga, Dar es Salaam. Jana usiku askari polisi walifika kwenye moja ya nyumba zilizopo eneo wakiambatana na viongozi wa mtaa ambapo, baada ya mazungumzo ya dakika kadhaa waliondoka na watu wanaelezwa kuwa ni wanafamilia.

Mwananchi limezungumza na baadhi ya majirani wa eneo hilo ambapo, wamezungumza namna wanavyomfahamu mtu waliyemtaja kwa jina la Hamza kwamba, alikuwa mpole na asiyependa kuzungumza.

Mmoja wa majirani hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Nabil, amesema amemfahamu Hamza tangu utotoni ni mpole na ameshangazwa na taarifa ya tukio hilo la mauaji.

“Tunamjua na siyo mzungumzaji anafanya kazi na  akija hapa anatoa salamu anapita njia mchezo umekwisha, hana mpya si mzungumzaji kwa sana, mtu wa kawaida hana matatizo na mtu nimeshangaa sana na wala sikutegemea kama anaweza kufanya kitu kama kile nimeshangaa hadi sasa hivi nashangaa,” amesema Nabil.

“Ukikaa naye ni mtu wa kawaida hana mazungumzo mengi, yeye ni mtu wa machimboni anaishi hapa tunamjua tangu utotoni,” Nabil

Kwa upande wake Issa, ambaye pia ni jirani wa kijana huyo ameeleza kuwa alikuwa anaishi eneo hilo na mama yake pamoja na ndugu yake, ambaye amedai kuwa hakumuona kwa muda wa siku mbili.

“Hapo kwao alikuwa anaishi na mama yake na kaka zake walikuwepo ila mmoja siku mbili hizi sijamuona nahisi atakuwa amesafiri,” amesema Issa.