Prime
Madai polisi kugeuza baa kitega uchumi
Dar/mikoani. Sakata la askari wawili wa Jeshi la Polisi wa Kituo cha Mabatini, Dar es Salaam kushikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya mlinzi wa baa maarufu jijini humo ya Board Room iliyopo Sinza, Razak Azan (29), limeibua mapya jinsi askari wanavyozigeuza baa na kumbi za starehe kuwa vitega uchumi vyao.
Tukio hilo lilitokea saa saba usiku wa kuamkia Jumatano ya Novemba 29, mwaka huu wakati askari hao wakitaka kumkamata mmoja wa wahudumu katika baa hiyo wakidai alikuwa anafanya biashara ya kujiuza.
Meneja wa baa hiyo, Frank Tukai alisema, askari hao walifika kwenye baa hiyo saa sita usiku na kutaka kumkamata mmoja wa wahudumu aliyekuwa akitoka kwenye duka jirani na baa hiyo.
Mmiliki wa baa hiyo alidai hilo halikuwa tukio la kwanza na kuwa askari wa jeshi hilo wamekuwa wakifika nyakati za usiku na kutaka wapewe “hela ya mafuta”.
Kutokana na tukio hilo, gazeti hili limefanya uchunguzi katika maeneo ya baa na kumbi za starehe Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha na Mbeya kubaini baadhi ya askari wamezigeuza vitega uchumi na kusababisha kero.
Imekuwa kawaida ukiwa baa au kumbi za starehe usiku kuona gari la polisi kufika na kuegeshwa eneo hilo na kupelekewa chochote na mameneja au wahudumu na wasipofanya hivyo, huona vitisho vya hapa na pale ikiwemo kutakiwa kufunga shughuli.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo, alimtaka mwandishi awasiliane na makamanda wa polisi wa mikoa inayolalamikiwa.
"Niko njiani hilo unalotaka kujua sina taarifa nalo, watafute makamanda wa mikoa ambayo umesikia hayo malalamiko," alisema Misime.
Katika maelezo yake kwa Mwananchi, Mkurugenzi wa baa ya Board Room, Frank Temba alisema wamekuwa wakitakiwa kutoa fedha kama sehemu ya kuchangia mafuta ya magari kwa ajili ya doria usiku.
Alisema gharama hizo zinategemeana na siku yenyewe lakini askari wamekuwa na utaratibu wakipita na kuchukua hela kwa ajili ya mafuta.
“Ni kweli askari huwa wanapitia kwenye hizi baa wakitaka hela ya chakula, kama huna wanataka kinywaji, huu utaratibu umeshazoeleka umekuwa kitu cha kawaida," alisema Temba.
Mbali na Temba, baadhi ya wamiliki wa baa waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, walidai kuwa kitendo cha askari Polisi kupita wakiwa na magari yao na kuchukua kuanzia Sh10,000 hadi 50,000 ni jambo linalowaumiza na kuwaongezea gharama ya uendeshaji kwani wanalipia leseni nyingi ikiwemo za halmashauri, afya, Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota), tozo ya huduma na nyingine zisizopungua 20.
Inaelezwa kuwa baadhi ya askari wakipita kwenye kumbi hizo wanakuwa wagumu wakihitaji fedha kama sehemu ya gharama ya mafuta ya kutia kwenye gari linalotumika kufanya doria na wanaokataa wanakamatwa.
Hata hivyo, wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, wadau na wamiliki za kumbi hizo walidai askari hao wanatumia udhaifu wa baadhi ya wamiliki na mameneja wa kumbi hizo kutokujua sheria na kuwatoza fedha kulingana na ukubwa wa biashara zao.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Baa na Kumbi za Starehe Tanzania (Ubakuta), Mponjoli Mwakabana alisema changamoto ya polisi kugeuza chanzo cha mapato imeanza muda mrefu ni utamaduni unaendelea kurithishwa na umekuwa ukiwaumiza.
“Kinachochangia watu kuingia kwenye mazingira hayo sheria zimekuwa ngumu, unakuta hadi inafika saa sita usiku muda wa kufunga hujafanya biashara, wakipita polisi unaongea nao wanakubali wanakudai kuwapa chochote kitu, pesa au vinywaji,” alisema.
Alisema katika mazingira hayo kuna siku zinapita hata gari saba katika ukumbi mmoja na kila gari lazima ipewe chochote kitu japo kuna baadhi yao ni waelewa, wakielezwa wanawasilikiza lakini wengine hawaondoki bila kupewa fedha au vinywaji.
Alisema Polisi wakipewa Sh5,000 wanakataa wataka kuanzia Sh10,000 huku akieleza gari zinazopita ni nyingi kuanzia saba kwa siku miaka ya nyuma wakati Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa aliwasaidia na ugomvi na askari ulipungua.
“Changamoto iliyopo Watanzania wengi wanaogopa polisi, wakija wakitishiwa kidogo wanatoa fedha na kwa kuwa hawajui sheria na ni changamoto kubwa tumeikuta na wanaendelea kuipitia,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Mkoa wa Mwanza, Patrick Masagati alisema chama hicho kimekuwa kikipokea malalamiko ya baadhi ya askari kwenda kula, kunywa bila kulipia na wakati mwingine kuomba fedha, japo hakutaja kiasi cha fedha.
“Hata hapa Mwanza tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa wamiliki wa baa wakilalamikia tabia za baadhi ya askari kwenda kwenye baa zao kula, kutumia vinywaji na vileo bila malipo hasa wakati wa doria za usiku,” alisema.
Alisema hawajui sababu za askari hao kuchukua fedha, kula na kunywa bure kwa kuwa wamiliki hao wanafanya biashara kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali za ufanyaji biashara hizo.
“Wakati mwingine wahudumu wa baa wanakamatwa usiku bila sababu lakini wakitoa pesa wanaachiwa, hii haifai na sisi kama jumuiya tulitaka tutoe tamko kuhusiana na suala hili,” alisema.
Alisema licha ya malalamiko ya wamiliki wa baa kumekuwa na tabia ya baadhi yao wakidai kuwa wananyanyaswa na vyombo vya ulinzi na usalama wakitaka fedha kinyume na utaratibu.
Akizungumzia hali wanayopitia, Yasinta Maleko ambaye ni muhudumu baa ya New Life Tabata, alisema suala la polisi kupita kwenye baa na kuchukua fedha limekuwa ni jambo la kawaida kama trafiki wanavyochukua kwenye dalaldala.
Alisema ukiacha polisi hata vikundi vya ulinzi shirikishi navyo vimekuwa vikipita kwenye baadhi ya maduka na baa usiku wakitaka kuchangiwa fedha, usipofanya hivyo inaonekana ni kosa," alisema Maleko.
Kwenye bendi
Mmiliki wa bendi ya muziki wa Dansi ya Tunda Spesho, Mwinjuma Muumini alisema askari kulipwa fedha, vyakula au vinywaji kwa baa wanazozungukiwa usiku wameugeuza mradi wao mkubwa.
Alisema malipo kwa polisi hao inategemeana na kiwango cha ukubwa wa biashara unayofanya lakini wastani wa kima cha chini wanaanza kuchukua kuanzia Sh10,000 hadi Sh40,000.
“Wakati mwingine wanaombwa kuongeza kama wakiwa wengi kwenye gari yao na wanaofanya mradi na wala hakuna siri na wanazunguka kuanzia saa tano usiku wakifika kwenye baa wanasimama nje halafu gari inawasha taa na kuzima meneja au mmiliki lazima utoke kuwapa chochote bila kufanya hivyo hawatoki,” alisema.
Alisema wakiona kiongozi kwenye baa husika hatoki anashuka mmoja wa kiongozi wa gari hiyo kuleta vitisho na mameneja wakiona hali hiyo wanaingia mfukoni kutoa chochote kitu.
“Hata sisi wapigaji wa bendi tunakuwa kwenye wakati mgumu, mwaka 2019 niliwahi kukamatwa na timu yangu yote ilikuwa siku ya Jumamosi ilipofika saa tano gari ya polisi likaingia, mwenye baa hakuwepo wala meneja tulichukuliwa kwenda Maturubai Mbagala,” alisema.
‘Tunahitaji usalama’
Meneja wa Bendi ya Msondo, Said Kibiriti alisema ni kweli katika kumbi hizo wanahitaji usalama japo kuna kasoro zilizojitokeza kwa askari kuanzisha utaratibu wa kuzungumza kwa siri na meneja au mmiliki.
“Unakuta si gari moja zinakuwa hata tatu akitoka moja inakuja nyingine imekuwa changamoto na unakuta gari hizo zimepangwa kufanya kazi kwa eneo (zone) tunapata mashaka sana kuna kiasi fulani huwa wanafuata wanapokuja kwenye kumbi,” alisema.
Alisema ingawa yeye hajawahi kupata changamoto hiyo kama mmiliki wa bendi lakini amekuwa akishuhudia mara kwa mara meneja na wamiliki wa baa kutoka na kuongea na polisi kila zinapokuja gari zao kwenye maeneo yao.
“Tunaona wanakuja kama wanavyofanya askari wa barabarani na makondakta wa daladala kinachozungumzwa hukijui mara unaona meneja anapeleka kadi au wanachukua kadi na kuondoka nazo, sasa hatujui mazungumzo yanakuwaje,” alisema.
Majibu ya Polisi
Pamoja na malalamiko hayo Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema halijapokea malalamiko yoyote ya kutozwa fedha na askari polisi wanaofanya doria usiku huku likidai kufuatilia kujua ukweli wake.
Akizungumza na Mwananchi, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Gabriel Puppa alisema: “baada ya kupata malalamiko hayo ngoja nifuatilie kwa kuongea na polisi kujua ukweli wake kwa sababu hakuna malalamiko niliyoletewa.”
Jijini Dodoma, mmoja wa wamiliki wa baa, Leonard Kisengi alisema askari polisi wamekuwa wakifika kwenye baa yake na kuanza kukagua vitu ambavyo haviwahusu huku wakiwa na lengo la kutaka pesa.
Alisema askari hao huwa wanafika majira ya saa 5 usiku ambao ni muda unaoruhusiwa kwa wauzaji wa vinywaji vikali na kuwataka wafunge biashara wakati wanaruhusiwa kufanya biashara hadi saa 6:00 usiku.
Naye Mathayo Simba kutoka Mbeya alisema askari ni walinzi wa usalama kwenye maeneo yao hasa kwenye baa ambazo zinauza vilevi ili kuhakikisha kuna usalama wa kutosha.
“Kwa sasa tunaona ni hali ya kawaida wakija askari kama wateja wamejaa ili wasisumbuliwe nalazimika kutoka nje kumalizana nao na kisha kurejea kuendelea na biashara na imekuwa kama sheria kwetu,” alisema Ester Damiani, mmiliki wa grosari eneo la Soweto jijini Mbeya.
Alisema kibaya zaidi muda wanaofika wanategea wateja wakiwa kwenye utulivu wa kupata kunywaji, kitendo ambacho kinasababisha kukimbia na fedha za vinywaji kwa kuhofu kukamatwa na polisi wanaokuwa doria wanapoingia kwenye vyumba vya biashara.
“Tunajikuta kuyumba mtaji ili kukwepa fedheha ya kufika kituo cha Polisi,tunaomba Serikali iliangalie hilo ili kurejesha nidhamu ya utendaji wa kazi na sio kuweke rushwa kama ni uhalali kwa wafanyabishara wa vileo. ”alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alikemea na kuonya askari kutojihusha na tabia hiyo kwani jukumu lao ni kufanya doria za kulinda usalama wa raia na mali zao.
“Tutaendelea kuelimishana kama yapo tutawashughulikia, kazi ya askari ni kulinda usalama wa raia na mali za zao na sio kuchukua rushwa ,niombe tu wananchi watakaopata changamoto hiyo kutoa taarifa ofisini kwangu,” alisema.
Imeandikwa na Fortune Francis, Tuzo Mapunda (Dar), Saada Amir (Mwanza), Janeth Mushi (Arusha), Rachel Chibwete (Dodoma) na Hawa Mathias (Mbeya).