Madaktari 10 watiwa kitanzini

Dar es Salaam. Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT), limewafungia leseni ya kutoa huduma madaktari sita, huku wanne wakipewa onyo kali baada ya kutiwa hatiani, kwa makosa ya ukiukwaji wa kanuni za maadili na utendaji wa kitaaluma.

Ukiukwaji huo umeelezwa kuwa ulichangia madhara kwa wagonjwa, ikiwamo kupata ulemavu na vifo.

Kufungiwa kwa leseni zao hakutawawezesha madaktari hao kutoa huduma za afya mpaka adhabu zao zitakapokwisha, ikiwa tu haitaamriwa kufutiwa kabisa leseni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa baraza hilo, Profesa David Ngassapa alisema uamuzi huo umetolewa baada ya kusikilizwa kwa mashauri tisa kati ya Januari 22 hadi 26, 2024.

Aliwataja madaktari kutoka vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya waliofungiwa leseni kuwa ni Vindhya Pathirana, Issa Nyangalaga, Aziz Mnkombe, Daniel Massawe, Getruda Mungale na Mulindwa Mazana.


Dk Massawe

Dk Daniel Massawe wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, amefungiwa leseni ya kutoa huduma kwa muda wa miaka miwili.

Atatakiwa kwenda mafunzo ya weledi, maadili ya kitaaluma na huduma kwa mteja katika hospitali maalumu kwenye kitengo cha upasuaji, kabla ya kurudishwa kutoa huduma baada ya muda wa kutumikia adhabu kumalizika.

“Ameamriwa kuacha mara moja kufanya huduma za upasuaji wa kibingwa wa mifupa hata atakapomaliza kutumikia adhabu,” alisema Profesa Ngassapa na kuongeza:

“Daktari huyu ameamriwa kugharimia matibabu ya wagonjwa Martha Mtega na Joseph Alphonce, ambao aliwasababishia ulemavu kutokana na upasuaji usioridhisha.”


Dk Vindhya

Alisema Dk Vindhya wa Kituo cha Afya Cradle kilichopo Msasani mkoani Dar es Salaam, amefungiwa kutoa huduma kwa muda wa miaka miwili.

“Daktari huyu ameelekezwa kuenda kwenye mafunzo ya weledi, maadili ya kitaaluma na huduma kwa mteja katika hospitali ya kufundishia kwa muda wa mwaka mmoja kwa gharama zake, kabla ya kurudishwa kutoa huduma baada ya muda wa kutumikia adhabu,” alisema.


Dk Nyangalaga

Kuhusu Dk Nyangalaga wa kituo cha afya Kibaoni kilichopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara, mkoani Morogoro, amefungiwa leseni kwa muda wa mwaka mmoja.

Dk Nyangalaga ameelekezwa kwenda mafunzo ya weledi, maadili ya kitaaluma na huduma kwa mteja kwa muda wa mwaka mmoja kwenye hospitali ya ngazi ya mkoa katika idara ya mama na mtoto, kwa gharama zake kabla ya kurudishwa kutoa huduma baada ya muda wa kutumikia adhabu.


Dk Mnkombe

Dk Mnkombe wa Hospitali ya Wilaya Mkuranga mkoani Pwani amefungiwa leseni kwa muda wa miezi sita.


Dk Mungale

Kwa upande wake, Dk Mungale wa Hospitali ya Wilaya Kigamboni, Dar es Salaam amefungiwa kwa muda wa miezi sita na ameelekezwa kwenda kwenye kliniki ya mafunzo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kitengo cha wagonjwa wa dharura kwa gharama zake, na kufanyiwa uchunguzi wa afya kabla ya kurudishwa kutoa huduma baada ya muda wa kutumikia adhabu.


Dk Mazana

Dk Mazana wa zahanati ya Kasulwa iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma naye amekumbwa na adhabu hiyo.


Waliopewa onyo

Waliopewa onyo ni Dk Living Colman wa Hospitali ya Saifee iliyopo wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Dk Rajah Chomboko wa Kituo cha Afya Kibaoni kilichopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara, mkoani Morogoro.

Mwingine ni Luma Kigota ambaye ni mtaalamu wa tiba kwa vitendo wa kituo binafsi cha Kilulu kilichopo wilayani Temeke na Dk Shafuri Ngaboli wa kituo cha afya Kabuku kilichopo katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Profesa Ngassapa alisema katika mashauri hayo pande zote mbili zilifahamishwa haki ya kukata rufaa kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 43(2),(3) na 44 cha sheria ya udaktari, udaktari wa meno na afya shirikishi.

Baraza limetoa rai kwa wanataaluma kuzingatia kanuni na maadili ya kitaaluma za mwaka 2005 na kanuni ya 3.2 ya kanuni za maadili na mwenendo wa kitaaluma kwa madaktari za mwaka 2005.


MAT yaonya madaktari

Kutokana na hatua zilizochukuliwa kwa madaktari hao, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimewasisitiza wanapofanya kazi yao kutumikia viapo vyao vyenye miiko na maadili.

Rais wa MAT, Dk Deus Ndilanha alisema wamekuwa wakiwasisitiza kuyaishi yale yaliyo katika viapo vyao ili yanapotokea makosa Baraza linajiridhisha kama kosa lingeepukika au lisingeepukika kama lipo ndani ya yale wanayofundishwa, hivyo kwa kuishi miiko ya kidaktari watapunguza malalamiko kutoka kwa wagonjwa.

“Dunia ya sasa inataka mrejesho kwa mgonjwa umpe taarifa, amekuja na tatizo gani, yeye alikuwa na fikra gani, ongea naye ajue ile tiba uliyompa ni kwa nini, usipofanya hivyo hizi kesi hazitaisha na sasa zinaanza kuwa nyingi. Wawe wawazi ili wagonjwa waelewe walichofanyiwa na ikibidi waweke katika maandishi,” alisema.

Dk Ndilanha alisema daktari anaweza kushtakiwa na mgonjwa au baraza kwa niaba ya Serikali ambalo kazi yake kubwa ni kuangalia na kuona ni kosa gani linaloweza kuepukika au limefanywa kwa makusudi.

“Baraza litajiridhisha aina ya kosa lililotendeka na aina ya adhabu anayoweza kupewa, baada ya uchambuzi wa muda mrefu, baraza linafanya uchunguzi inatumwa timu na baadaye linakaa kujadili na kufanya maamuzi,” alisema.


Makosa yaliyowatia hatiani

Msajili wa Baraza la Madaktari, Dk David Mnzava akitoa ufafanuzi wa makosa ya madaktari hao alisema:

Dk Vindhya, ametiwa hatiani baada ya kumzidishia mgonjwa dawa aina ya Methotrexate licha ya kushauriwa.

Pia alizuia mgonjwa kupatiwa rufaa kwa wakati alipozidiwa, hivyo kusababisha kifo cha mgonjwa.

Dk Colman alipewa onyo baada ya kuchelewa kumhudumia mjamzito

aliyepata changamoto wakati wa kujifungua na kusababisha kupoteza damu nyingi, hali ilisababisha kifo chake.

Dk Nyangalaga ametiwa hatiani baada ya kuondoka kituoni wakati akiwa zamu bila kutoa taarifa na kusababisha kifo cha mjamzito baada ya kukosa huduma.

Dk Chomboko ametiwa hatiani baada ya kushindwa kumpa huduma stahiki mjamzito na kumpa rufaa kwa wakati, hivyo kusababisha kifo chake.

Dk Mnkombe ametiwa hatiani kwa kushindwa kumhudumia mjamzito aliyehitaji huduma ya dharura, hivyo kuchangia kifo chake.

Dk Ngaboli alitiwa hatiani baada ya kushindwa kumhudumia mjamzito kutokana na kuwa nje ya kituo huku akiwa zamu

Pia kushindwa kumpa rufaa kwa wakati na kusababisha afariki dunia akiwa kituoni hapo.

Dk Massawe alikutwa na hatia kwa kutoa huduma ya upasuaji wa mifupa nje ya utaratibu wa taaluma yake, ambayo haimruhusu kutoa huduma hiyo, hivyo kuwasababishia ulemavu wagonjwa.

Dk Kigota alikutwa na hatia baada ya kutoa huduma ya tiba kwa vitendo katika kituo kisichosajiliwa na bila kufuata miongozo stahiki ya kutoa huduma, kinyume na Kanuni za Maadili Kitaaluma

zinazomtaka mtoa huduma kuzingatia utu na heshima kwa mgonjwa.

 Dk Mungale akiwa zamu alishindwa kuwahudumia kikamilifu wagonjwa na kushindwa kuwapa rufaa.

Kwa upande wake, Dk Mazana aliamriwa kuendelea kutumikia adhabu ya kufutiwa leseni baada ya maombi yake ya mapitio ya

hukumu kutupiliwa mbali, baada ya kumfanyia upasuaji mkubwa mgonjwa katika zahanati kinyume cha miongozo ya utoaji huduma na hivyo kumsababishia mgonjwa madhara makubwa.