Madaktari watatu waliosababisha vifo mama, mtoto wafutiwa usajili

Muktasari:

  • Madaktari watatu wamesimamishwa kazi na kufutiwa usajili baada ya kubainika kufanya uzembe na kusabisha vifo vya mama na mtoto wakati akijifungua katika hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

Unguja. Madaktari watatu wamesimamishwa kazi na kufutiwa usajili baada ya kubainika kufanya uzembe na kusabisha vifo vya mama na mtoto wakati akijifungua katika hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Baraza la Madaktari Zanzibar kufanya uchunguzi kwa takribani wiki moja na kuwatia hatiani Madaktari hao huku mwingine mmoja akinusurika baada ya uchunguzi kubaini hana hatia.

Tukio hilo lilitokea Mei 15, 2023 hospitalini hapo baada ya mama huyo, Kidawa Haji Khamis Mwalimu wa Shule ya Kidongochekundu ambaye alifika kwa jili ya kujifungua, hata hivyo inadaiwa kuwa kutokana na uzembe wa madaktari hao walifariki dunia.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Mei 25, 2023 Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh amewataja madaktari hao kuwa ni Daktari bingwa wa wagonjwa wa dharura Nihfadh Issa Kassim, Salamuu Rashid Ali na Riziki Suleiman Yussuf ambaye pia amebainika hana leseni ya udaktari kisiwani hapo.

Naibu Waziri Hafidh amesema kosa la Dk Salamuu ambaye alikuwa zamu siku hiyo katika wodi ya wazazi, ni kushindwa kumpa kipaumbele mwanamke huyo licha ya kufahamu kwamba mgonjwa huyo alihitaji huduma za haraka, huku akitoa taarifa za kughushi baada ya kutokea kifo cha mama huyo.

“Baada ya uchunguzi wa baraza la madaktari limebaini makosa hayo na hivyo limeamua kumfutia usajili kwa muda wa mwaka mmoja,” alisema.

Kwa upande wa Dk Nihfadh, taarifa zimesema kuwa uchunguzi wa Baraza umegundua alikiuka kanuni ya 9 ya maadili hivyo limeamua kumfutia usajili kwa muda wa miaka miwili.

“Huyu daktari alishindwa kufanya mamuzi sahihi akiwa kama daktari bingwa wa magonjwa ya dharura na kushindwa kusimamia haki ya mgonjwa kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi baada ya kufanyiwa upasuaji,” alisema.

Amesema katika uchunguzi huo, umebaini pamoja na kushindwa kutumiza wajibu wa kumhudumia mgonjwa pia umebainika kuwa alikuwa anafanyakazi bila kuwa na leseni ya Baraza la Madakatari Zanzibar.

“Hivyo amefanya kosa kinyume na kifungu cha 17(1) na 22(1) cha sheria ya madkatari tiba na madkatari meno Zanzibar namba 12 ya mwaka 1999 hivyo Baraza limeamua kuchukua hatua kumripoti polisi kwa hatua za kijinai,” alisema.

Awali idadi ya madaktari hao ilikuwa wanne, lakini baaada ya Baraza kufanya uchunguzi limebaini Dk Masoud Omar Hamad hana hatia yoyote kwani siku ya tukio alikuwa chumba cha upasuaji.

Naye Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara hiyo, Dk Msafiri Marijan alisema aliwataka watendaji kubadilika kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Amesema wakati mama huyo alipofika hapo tena akiwa anahitaji huduma za dharura hawakuwa na kazi zilizowabana lakini ni kwasabu ya kutokujali na kufanya kazi kwa mazoea.