Madakrati bingwa 24 kuweka kambi Simiyu

Muktasari:

  • Madaktari bingwa 24 wanapelekwa Simiyu kuweka kambi ya siku tano kwa ajili ya kusaidia wananchi kupata huduma za kitabibu.

Dodoma. Madaktari bingwa 24 wanapelekwa Simiyu kuweka kambi ya siku tano kwa ajili ya kusaidia wananchi kupata huduma za kitabibu.

 Taarifa ya Katibu wa Afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu Jackson Mjinja iliyotolewa leo Mei 22, 2023 imeeleza kuwa, maandalizi kwa ajili ya kambi hiyo yameshakamilika.

Madaktari hao wataanza kambi hiyo Juni 5 hadi 9, 2023 na watafanya kazi ya uchunguzi, tiba na ushauri katika kambi hiyo kwa mashirikiano na madaktari wa hospitali.

Mjinja amesema Mganga Mfawidhi wa Hopsitali ya Rufaa ya Mkoa huo, Dk Athanas Ngambakubi ataongoza kambi hiyo ambayo itafanya kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi hasa kwenye magonjwa yanayowahitaji madaktari bingwa.

“Tumekamilisha maandalizi yote katika Kambi hii maarufu Mama Samia Suluhu Hassan, madaktari watakaokuwepo wote ni mabingwa na wabobezi kwenye kada hii, tunaomba wananchi wajitokeze wka wingi kupata huduma hii,” amesema Mjinja.

Katibu amesema kambi hiyo ambayo inagharamiwa na Serikali kupitia gharama za moja kwa moja kutoka mfuko wa Rais, itajihusisha zaidi na magonjwa ambayo yanahitaji wabobezi.