Madaktari bingwa 32 kutoka China watua Zanzibar
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza katika hafla ya kuitambulisha timu ya madaktari madaktari bingwa 32 kutoka China Ikulu jana Februari 8, 2023
Zanzibar. Timu ya madaktari bingwa 32 kutoka China wameanza kutoa huduma za kibingwa katika Hospitali za umma kisiwani Zanzibar.
Wataalamu hao watakuwa Zanzibar kwa mwaka mmoja wakitoa huduma za macho, meno, upasuaji kwa wanawake kwa kutumia tundu dogo, uzazi, saratani na magonjwa mengine ya wanawake wakishirikiana na wenzao wa kisiwani humo.
Akizungumza katika hafla ya kuitambulisha Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi Ikulu jana Februari 8, 2023 kiongozi wa madaktari hao Dk Zhao amesema imani yao watapunguza changamoto za maradhi hayo yanayowasumbua wananchi kisiwani humo.
“Kikubwa wananchi waitumie fursa hii kufika kwa wingi kwenye hospitali za umma ili wapate matibabu na ushauri wa kitaalamu,” alisema Dk Zhao
Naye Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya, Dk Msafiri Marijani amesema mbali na matibabu kwa wananchi lakini kuanzishwa kitengo cha madaktari bingwa watakaofanya operesheni bila ya kumpasua mgonjwa katika hospitali za Mnazi Mmoja na Abdalla Mzee.
Amesema kwa mara ya kwanza Mnazimmoja wametumia upasuaji bila kupasua ambao ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa sambamba na kusifu vifaa vipya vya kitaalaamu kutoka kwa timu hiyo aliyoieleza kwamba imeongeza uweledi na ufanisi wa hali ya juu.
Naye Rais Mwinyi alisema ujio wa timu ya madaktari hao ni faraja na fursa adhimu ya kuimarisha sekta ya afya Zanzibar.
Amesema ushirikiano uliopo baina ya China na Zanzibar ni wa kihistoria na wa muda mrefu na aliishukuru China kwa kuendelea kuiungamkono Zanzibar hususani kwenye sekta ya afya, kwa msaada wa vifaa vya kisasa na teknolojia mpya ya kufanya operesheni bila upasuaji pamoja na huduma nyingine za uchunguzi na kitabibu.
Dk Mwinyi aliiomba serikali ya China kuendelea kuisaidia Zanzibar madaktari bingwa kwani serikali imejiimarisha zaidi kwenye sekta ya afya kwa kuongeza hospitali za wilaya Unguja na Pemba hivyo na kuwaomba madaktari hao kuongeza nguvu na utaamu kwenye hospitali hizo.
Naye balozi mdogo wa China, Zhang Zhisheng aliyeambatana na timu hiyo amempongeza Rais Mwinyi kwa kuiongoza Zanzibar kuwaletea maendeleo wananchi wake na kueleza wanashuhudia mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Timu hiyo ya madaktari bingwa 32 kati yao 12 watashirikiana na madaktari wazawa kwenye Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja na wengine watakwenda kuongeza nguvu kwenye hospitali ya Abdalla Mzee, Pemba.