Madaktari bingwa watua Mbeya kutibu macho

Wananchi wa maeneo mbalimbali jijini Mbeya wakiwa wamejitokeza kwa ajili ya uchunguzi wa awali wa matibabu ya macho kupitia Taasisi ya Bilal Missionary Tanzania  na kupatiwa huduma bure ikiwepo miwani, oparesheni ndogo na mtoto wa jicho. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

Huduma hizo zimeanza kutolewa leo Ijumaa Desemba 9, 2022 na taasisi ya Bilal Muslim Mission Tanzania kwa kushirikiana na kupitia taasisi ya Tulia Trust ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru.

Mbeya. Zaidi ya wananchi 3,600 mkoani Mbeya   wanatarajia kufanyiwa uchunguzi wa awali na matibabu ya macho ikiwepo mtoto wa jicho na kufanyiwa operesheni ndogo na kupatiwa miwani bure.

Kazi hiyo imeanza leo Ijumaa Desemba 9,2022 kupitia taasisi  Bilal Muslim Mission Tanzania kwa kushirikiana na taasisi ya Tulia Trust ambayo Mkurugenzi wake ni  Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Akizungumza na Mwananchi katika utoaji wa tiba hiyo, mratibu wa taasisi hiyo, Ain Sharrifi amesema kuwa matarajio yao ni kufanya uchunguzi wa awali na matibabu kwa wagonjwa 1,200 kwa siku na watakaokutwa na magonjw aya macho watapatiwa matibabu bure.

“Tumefika mkoani Mbeya kupitia Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na tumeona mwamko wa wananchi ni mkubwa, hivyo matarajio kwa siku ni  kuhudumia wagonjwa 1,200 na lengo ni kufikia zaidi 3,000 kwa siku tatu tutakazokuwa hapa,” amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Taasisi ya Tulia Trust, Jackline Boaz amesema kuwa ni wakati sasa wananchi wa Mbeya kutumia fursa hiyo kupata uchunguzi wa awali wa matatizo ya macho na kupatiwa matibabu bure katika viwanja vya Ruanda Nzovwe.

“Tumepokea Madaktari bingwa 40 wa macho kutoka taasisi ya  Bilal Muslim Mission Tanzania kutoka Jijini Dar es Salaam kwa muda wa siku tatu tuna imani mambo yanakwenda vizuri sambamba na  kutoa kipaumbele  kwa wazee na walemavu,” amesema.

Naye Ofisa uhusiano wa Tulia Trust, Joshua Mwakanolo amesema kumekuwepo na mwamko mkubwa kwa wananchi kujitokeza ambapo mpaka sasa kwa makadirio zaidi ya watu 2,000 wamejitokeza.

Mkazi wa Isanga Jijini Mbeya ambaye amepatiwa matibabu ya miwani bure, Bupe Mwaisaka ameshukuru kwa huduma hiyo na kwamba alikuwa na changamoto ya maumivu ya kichwa mara kwa mara.