Madaktari wa meno wasema wako hatarini zaidi kuambukizwa corona

Madaktari wa meno wasema wako hatarini zaidi kuambukizwa corona

Muktasari:

  • Wakati janga la corona likiendelea kutikisa dunia, Chama cha wataalam wa Afya ya Kinywa na Meno Tanzania (TDA) kimewataka madaktari wa meno kuongeza umakini wakati wa utoaji huduma kwa kuwa kundi hili lipo hatarini zaidi kuambukizwa.


Dar es Salaam. Wakati janga la corona likiendelea kutikisa dunia, Chama cha wataalam wa Afya ya Kinywa na Meno Tanzania (TDA) kimewataka madaktari wa meno kuongeza umakini wakati wa utoaji huduma kwa kuwa kundi hili lipo hatarini zaidi kuambukizwa.

Hii ni kutokana na wataalam hao kufanya kazi kwa ukaribu na kinywa huku matibabu yake wakati mwingine huwa chanzo cha kutengeneza matone ya mate yanayoruka kutoka kinywani na kuweza kuwa chanzo cha kusambaa ugonjwa huo.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 4, 2021 Rais wa TDA  Dk Deogratius Kilasara amesema tangu wimbi la tatu kuingia  chama hicho kimeshapoteza wanachama watatu kutokana na ugonjwa huo.

Amesema  eneo wanalofanyia kazi ndio kiwanda cha kusambaza ugonjwa huo hivyo ni muhimu kwao kuongeza tahadhari kwa ajili ya kujilinda na kuwalinda wengine.

Kufuatia hilo Dk Kilasara amewataka wataalam wa kinywa na meno kutumia fursa iliyotolewa na serikali ya kupata chanjo katika makundi ya kipaumbele.

“Ni ukweli usiopingika kuwa njia kuu ya maambukizi ya corona ni kupitia kuvuta hewa iliyoambatana na majimaji yaliyosambazwa kwa njia ya chafya au kupumua kupitia kinywa cha mtu mwenye maambukizi.

“Niwaombe wanatasnia watumie fursa hii kuchanja, chanjo hii ni salama kwa kuwa imechunguzwa na kuthibitishwa na mamlaka husika. Litakuwa jambo la kusikitisha kumpoteza mwanatasnia mwingine kwa kuwa sasa tuna njia ya kuzuia hilo,” amesema Dk Kilasara.