Madaktari waeleza jinsi ya kuikabili nimonia

New Content Item (1)
Madaktari waeleza jinsi ya kuikabili nimonia

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya wameeleza namna ugonjwa wa homa ya mapafu ‘nimonia’ ambao umekuwa ukitajwa kuwapata watu kadhaa nchini, unavyoambukiza, dalili zake na kutoa mbinu za kujikinga nao.
  • Kwa mujibu wa wataalamu hao, nimonia zipo za aina nyingi kulingana na visababishi vyake kama bakteria, virusi, kemikali, fangasi au zinazotokea iwapo chakula kimeingia njia ya hewa.

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameeleza namna ugonjwa wa homa ya mapafu ‘nimonia’ ambao umekuwa ukitajwa kuwapata watu kadhaa nchini, unavyoambukiza, dalili zake na kutoa mbinu za kujikinga nao.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, nimonia zipo za aina nyingi kulingana na visababishi vyake kama bakteria, virusi, kemikali, fangasi au zinazotokea iwapo chakula kimeingia njia ya hewa.

Hayo yamebainika katika mahojiano maalumu na Mwananchi, madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mfumo wa hewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Elisha Osati na Dk Nakiganda Mkasa wa Hospitali ya Aga Khan pamoja na Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya, Dk Leonard Subi kuhusu ugonjwa huo.

Dk Nakiganda alisema ugonjwa huo husambaa kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya hewa, iwapo mtu mwenye uambukizo atapiga chafya au kukohoa ndipo vimelea huingia katika mfumo wa mtu mwingine kupitia pua au mdomo na vikaenda katika njia ya chini ya mapafu na kutengeneza maambukizi.

“Ukiwa umepata maambukizi katika njia ya juu ya hewa, labda una mafua ya aina fulani, matemate au makohozi yakaingia katika njia ya hewa upande wa chini (kwenye mapafu).”

Dk Nakiganda anasema hiyo inaweza kutokea kwa mtoto iwapo alikuwa na maambukizi ya mafua au mfumo wa juu wa hewa kisha yakashuka chini, hupata maambukizi ya nimonia.

Alisema wapo ambao hupata nimonia kwa kumeza, hasa ambao hupoteza fahamu, wakitapika vile vyakula vinaweza kuingia katika mfumo wa hewa na wakapata nimonia.

“Lakini kubwa ni kwa njia ya hewa, ndiyo maana tunashauri mtu apige chafya pembeni au azibe mdomo.”

Akifafanua zaidi Dk Nakiganda anataja aina za nimonia, “Nimonia unaweza kuiweka kwenye makundi mbalimbali lakini kwavijidudu vinavyosababisha kuna bakteria, virusi au fangasi.”

“Kuna (nimonia) unayoipata katika jamii, pia ipo nyingine ambayo unaipata katika hospitali sema tu vile vijidudu vinavyosababisha ndiyo vinakuwa tofauti,” aliongeza.

Dalili za nimonia

Dk Osati alisema mara nyingi wagonjwa huanza kukohoa na hapo tayari huwa imefika kwenye mapafu, kinaanza kikohozi kikavu baadaye kinatoa makohozi.

Alisema mgonjwa mara nyingi akishapata kikohozi huanza kuwa na homa kwa sababu wadudu wakiingia kwenye mapafu mwili huanza kupambana.

“Mwili unaanza kutoa kinga ambazo zinaanza kupambana na wale wadudu kwa hiyo katika yale mapambano inasababisha homa kutokea, mwili kuchoka na wengine wanakuwa na shida ya kupumua,” alisema Dk Osati.

Hata hivyo, Dk Osati alisema tatizo la kupumua linategemea ukubwa wake au udogo wake kulingana na mapokeo kwenye mwili.

Alisema mgonjwa anapojisikia hali ya kushindwa kupumua vizuri ni dalili anaweza kuanza kuchukua hatua za kunywa vinywaji vya moto, mchanganyiko wa limao, tangawizi, kama inavyoelekezwa. “Kwetu kama madaktari hatuoni ni jambo baya,” aliongeza.

Jinsi ya kujikinga

Dk Osati alisema ni lazima kuzingatia usafi wa mazingira, kunawa mikono kwa maji na sabuni, kutumia sanitaiza kwa kuwa wadudu wengi wanaingia kupitia mikono, kuvaa barakoa na kuepuka kugusana na watu. “Barakoa ni muhimu, ninapohudumia watu hapa kliniki lazima niwe nimevaa, tuepuke pia mikusanyiko,” alisisitiza.

Alisema watu wanatakiwa kuepuka kukaa katika upepo mwingi na kunywa vitu vya baridi sana.

“Vile virusi vimezoea kukaa kwenye joto fulani, ukinywa maji baridi joto likipungua inawafanya wale wadudu wanakimbia wanaingia kwenye mapafu kwa hiyo inasababisha nimonia. Tunashauri watu wanywe vinywaji vya moto, kujifukiza na usikae kwenye baridi,” alisema.

Dk Osati alisema asilimia kubwa ya wagonjwa wanaotibiwa mfumo wa hewa, waliofanya mazoezi walipona haraka kuliko waliolala muda mwingi.

Akielezea kinga, Dk Nakiganda alisema yeyote anayepata maambukizi hutegemea mfumo wa kinga wa mwili wake ukoje, lazima hivyo vitu viwili viwe katika uwiano.

“Ndiyo maana homa ya mapafu huwapata watoto chini ya miaka mitano na wazee zaidi ya miaka 60 kutokana na kinga zao za mwili,” alisema akiongeza kuwa vyakula au virutubisho vinaweza kutumika kuimarisha kinga na afya kutokana na aina za nimonia,” alisema Dk Nakiganda huku akionya kuhusu unywaji pombe kupindukia na uvutaji wa sigara kwa sababu vinaharibu kinga za mwili.

Mgonjwa afanye haya

Dk Osati anashauri kuwa hata kama pumzi inakata, mgonjwa atembee na iwapo atalala sana hali inakuwa mbaya zaidi, kwa hiyo ni muhimu atembee.

Alisema katika kulala inategemea mgonjwa anajisikia vizuri akilalia upande upi.

“Mara nyingi pafu la kulia huanza kushambuliwa zaidi ya la kushoto, pia tunashauri mgonjwa atumie mto au kitanda kiwe kimenyanyuliwa angalau nyuzi 45 kama unaweza kidogo kwa juu, kwa sababu inamsaidia mtu kunyanyua mapafu hewa iweze kupatikana vizuri,” alisema.

Dk Osati aliongeza kuwa mgonjwa akitumia mto humsaidia majimaji kutuama sehemu ya chini.

“Mara nyingi maji hujikusanya kwenye mapafu kwa chini, kwa hiyo ukilala chali moja kwa moja maji yanasambaa kwenye mapafu, ukikaa kifua umekinyanyua kidogo yanakwenda chini na yanasaidia mzunguko wa hewa kidogo kuliko kulala chali,” alisema.

Mkurugenzi Kinga

Akizungumzia pia ugonjwa huo, Dk Subi, mkurugenzi wa Idara ya Kinga, alisema kwa nimonia zinazosababishwa na virusi au bakteria ni vema mgonjwa kujikinga ili asisambaze vile virusi na kuleta maambukizi kwa wengine. “Inategemea na aina ya wadudu kama unawatoa kupitia makamasi au hewa, tunashauri mgonjwa ajikinge iwe ni kwa barakoa au kitambaa, ukijisikia una tatizo hilo unapoingia sehemu za watu hakikisha unachukua tahadhari kwa kunawa mikono kwa maji safi na sabuni,” alisema Dk Subi.

Alisema katika hizo zipo nimonia ambazo haziathiri mtu mwingine kimaambukizi.

“Nimonia ni madhara ya maambukizi chini ya mapafu lakini pia kuna uambukizi wa juu ambao ukishuka chini sasa ndiyo inakua nimonia na kwa zile zinazoambukiza ni kwamba wadudu ndiyo wanaambukiza vinavyotoka ni virusi au bakteria ndiyo maana tunashauri mgonjwa anapokaa katika mazingira ya watu ajikinge,” alisema Dk Subi.