Madalali wa mazao Makete washtukiwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Makete, William Makufwe akikagua upakiaji wa viazi ili kubaini wale wanaoweka lumbesa.
Muktasari:
- Waonywa kuwalazimisha wakulima kufunga lumbesa, wakidai soko linataka hivyo.
Njombe. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, William Makufwe ameshtukia mchezo aliouita mchafu wa madalali wa mazao wilayani humo.
Amesema baadhi yao huwashawishi wakulima kufunga lumbesa mazao yao wanapowauzia, jambo lisilokubalika kuwa wanawanyonya na kuwasababishia hasara kubwa.
Mkurugenzi huyo amesema hayo leo Ijumaa Julai 19, 2024 baada ya kuwatembelea wakulima wa viazi wa vijiji vya Kipagalo na Bulongwa wilayani Makete Mkoa wa Njombe.
Amesema wapo baadhi ya madalali huwalazimisha wakulima kuweka lumbesa kwa madai kuwa soko ndiyo linataka hivyo, jambo ambalo si sahihi.
Amesema madalali wanatakiwa kuwa na huruma kwa kuwa wakulima wanatumia gharama kubwa tangu wanapoanza maandalizi ya shamba mpaka wanapovuna.
"Tunavyofahamu Makete ishu huwa ni wale madalali, ndiyo wanawalazimisha wakulima kuweka lumbesa hapana, madalali tuwe na huruma na wakulima,” amesema Makufwe.
Amesema viazi ni moja ya zao linalowapatia wakulima wilayani humo fedha nyingi na halmashauri hiyo hupata fedha hizo kupitia ushuru wa mazao.
Amesema Julai ni kipindi ambacho bei huwa nzuri kwa kuwa viazi vinatoka maeneo machache ya wilaya hiyo (vijiji vya Kipagalo na Bulongwa).
Hata hivyo, amewapongeza wakulima wilayani humo kwa kuendelea kuchangamkia fursa ya kilimo cha viazi kwa kuwa kimeendelea kuwapatia kipato na kubadili hali zao za maisha.
Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Aniceth Ndunguru amesema mikakati waliyoweka kukabiliana na lumbesa ni kutenga vituo vya kukusanyia mazao katika maeneo yote ambako viazi vinalimwa.
Amesema katika vituo hivyo wakulima wanaelekezwa namna ya kutumia mizani kwa kuhakikisha mzigo huo hauzidi kilo 100 na elimu hiyo imeanza kutolewa tangu mwaka jana.
"Tunashukuru uelewa wa wananchi unakwenda taratibu wapo ambao wameelewa mifuko ile haizidi kilo mia na hili tumekubaliana kulifanya wote wa nyanda za juu kusini" amesema Ndunguru.
Amesema wanaokiuka sheria kwa kuweka lumbesa katika halmashauri hiyo adhabu yake ni kulipa Sh100,000 licha ya Baraza la Madiwani kuona faini hiyo ni ndogo.
Mnunuzi wa viazi kutoka Kampuni ya East Africa, Isack Sanga amesema kampuni hiyo inakataza kufunga lumbesa na wanafanya hivyo kwa masilahi ya wakulima na kampuni yenyewe.
"Biashara inakuwa nzuri endapo kila mmoja ataridhika na sidhani kama itakuwa sahihi umeshona viazi umepata faida, huku mkulima ananung'unika," amesema Sanga.
Baadhi ya wakulima wa viazi mkoani Njombe, akiwemo Oliver Mwani amesema lumbesa inawarudisha nyuma kwa sababu wanafunga mzigo mkubwa kuliko fedha wanayolipwa.
"Bei zinakuwa tofauti ukiweka lumbesa viazi, wananunua kwa Sh55,000 kwa gunia, lakini kilo 100 wananunua kwa Sh52,000 kwa gunia, kwa kweli tunaumia sana sisi wakulima,” amesema Mwani.