Madereva wa malori Tunduma wahofia usalama wao Tunduma

Muktasari:
- Sakata la mgomo wa madereva wa malori katika mpaka wa Tunduma umeendelea leo kwa siku ya pili ambapo baadhi ya madereva wasiounga mkono mgomo huo wameegesha magari yao kwa hofu ya usalama wao na magari.
Songwe. Sakata la mgomo wa madereva wa malori katika mpaka wa Tunduma umeendelea leo kwa siku ya pili ambapo baadhi ya madereva wasiounga mkono mgomo huo wameegesha magari yao kwa hofu ya usalama wao na magari.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Jumanne Julai 26, 2022 madereva hao wamesema licha ya kuwa Serikali imewahakikishia usalama wao lakini wanahofia kudhuriwa na wenzao wanaodaiwa kuhamasisha mgomo huo.
Mmoja wa madereva hao Justin Chaunga amesema wao wasiounga mkono mgomo huo bado hawajawa na uhakika na usalama wao kutokana na hofu.
" Bado tunahofu tunaweza kuzuiliwa njiani na tukadhurika ingawa kuendelea kubaki hapa tunaingia gharama nyingine kubwa" amesema Chaunga
Akizungumza na madereva hao kwa lengo la kuwahamasisha waendelee na safari zao Mkuu wa Mkoa Songwe, Omary Mgumba amewahakikishia usalama madereva hao.
"Kuhusu usalama wenu ni jukumu la Serikali Kikatiba kulinda raia wake na mali zao hivyo popote wanapokwenda wako salama Serikali pande zote tupo imara" amesema Mgumba.