Madereva wafunguka makosa feki barabarani

Madereva wafunguka makosa feki barabarani

Muktasari:

  • Msako wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani uliofikia siku ya sita, umeibua hoja za madereva ambao licha ya kuunga mkono, wamelitaka jeshi hilo lijikite katika kufanya uamuzi wa busara kwa makosa yanayosameheka na kuepuka kubambikia makosa kwa nia ya kuchochea rushwa.

Dar es Salaam. Msako wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani uliofikia siku ya sita, umeibua hoja za madereva ambao licha ya kuunga mkono, wamelitaka jeshi hilo lijikite katika kufanya uamuzi wa busara kwa makosa yanayosameheka na kuepuka kubambikia makosa kwa nia ya kuchochea rushwa.

Jeshi hilo lilianza operesheni yake Januari 20, mwaka huu kwa ajili ya kukamata magari yaliyolimbikiza faini na tozo zinazotokana na adhabu walizoandikiwa madereva barabarani.

Jana gazeti hili lilizungumza na madereva mbalimbali wa magari binafsi, wafanyabiashara ya usafiri wa abiria na malori yanayosafirisha mizigo, wakisema adhabu nyingi zinazotolewa zinachochea mazingira ya rushwa, hivyo wamelitaka jeshi hilo kujikagua na kuthibiti maofisa wasiokuwa waadilifu barabarani.

Augustine Malango, dereva wa daladala ya Masaki-Simu 2000 amesema, “kwa mfano ninadaiwa Sh30,000 nakutana na askari anakagua kweli anakuta nadaiwa, pale pale anaweza kukuandikia deni jipya kwenye mfumo bila kujua hadi utakapokutana na askari mwingine.”

“Ukikutana na askari mwingine ndio atakwambia siku, saa na eneo fulani ulipigwa faini, ukivuta kumbukumbu unamkumbuka aliyekukagua siku hiyo, hii inatokea sana na inaumiza wengi,” aliongeza.

Hata hivyo, Yasin Ally, dereva wa malori ya usafirishaji wa bidhaa za Azam katika mikoa mbalimbali nchini aliunga mkono operesheni hiyo akisema baadhi ya madereva wanachafua heshima ya madereva njiani.

“Kuna madereva wanabadilisha namba za magari ili kukwepa madeni yao, sasa hii inatufanya tuonekana wahuni,” aliongeza Yassin.

Dereva wa kampuni nyingine inayosafirisha bidhaa nchi jirani, aliyeomba kuhifadhiwa jina lake alisema kila anapoanza safari amekuwa akiandaa 40,000 kwa ajili ya kuzigawa kwa askari wa usalama barani ili kuondoa usumbufu wa kuchelewa mzunguko wa safari zake.

“Sisi tunalipwa kwa mzunguko wa safari, kadri tunavyowahi kupeleka mzigo na kurudi ndipo tunapoweka mazingira ya kulipwa posho nzuri ofisini, kwa hiyo ukijifanya mjuaji njiani trafiki anaweza kuifanya safari yako utumie siku nne au tano badala ya siku tatu.

“Yaani sasa hivi kuna tochi zinatuumiza sana njiani, mtusaidie, kwa mfano kuna mahali unatembea mwendokasi wa kilometa 50 kwa saa lakini unasimamishwa unaambiwa 60, maana yake ujiongeze mwenyewe, kwa kuwa nataka posho ofisini, nijenge heshima kwa bosi inabidi niwatulize trafiki kwa pesa,” alieleza dereva huyo mkazi wa Dar es Salaam.

Malalamiko yao yawagusa pia wenye magari ya madogo ya mazigo maarufu kama Kirikuu na bajaj ambao hawawezi kumaliza safari bila kusimamishwa na trafiki na hivyo kuwapotezea muda na fedha nyingi.

Wakati msako huo ukiendelea, Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Wilbroad Mutafungwa jana alieleza tathmini ya wiki moja, akisema imekuwa na mafanikio.

Hadi kufikia jana tayari jeshi hilo lilikuwa limekusanya Sh1.4 bilioni ikiwa ni sehemu ya malimbikizo ya faini na tozo ya karibu Sh12 bilioni.

Makusanyo hayo yanatokana na magari 24,521 ambayo madereva na wamiliki wake wamelipia.

Kwa takwimu hizo ni kuwa wastani wa magari 4,900 yanakamatwa kila siku katika mikoa mbalimbali na kuwezesha jeshi hilo kukusanya wastani wa Sh280 milioni kila siku.

Katika ufafanuzi, Mutafungwa aliwaambia wanahabari kuwa fedha hizo zimekusanywa tangu Januari 20, mwaka huu ilipoanza operesheni hiyo kwa kukagua magari mitaani, maeneo ya maegesho, gereji au maeneo ya wazi.

Operesheni hiyo ni agizo la Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro la Januari 6, mwaka huu kuhusu kuwapo mchezo wa madereva kubandua namba za magari yanjayodaiwa na kuweka katika magari yasiyodaiwa ili kuyatumia kukwepa kukamatwa.

Katika faini hizo, dereva anatakiwa kulipa faini ya Sh30,000 kwa kosa moja ndani ya siku saba. Muda huo ukipita bila kulipa, deni hilo kuongezekakwa Sh7,500 na huendelea kukua kwa kiwango hicho kila baada ya siku saba hadi itakapofikia ukomo wa Sh60,000.