Prime
Madereva wanavyoweka ‘roho mkononi’ wakisafirisha sulphur
Muktasari:
- Usafirishaji wa sulphur kwenda Zambia na DRC umeongeza shughuli za kiuchumi nchini, lakini baadhi ya madereva wanaeleza hofu kuhusu usalama wao.
Dar es Salaam. Kwa nje, huonekana kama safari nyingine ya kawaida ya kusafirisha sulphur kutoka Bandari ya Dar es Salaam kuelekea Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Lakini nyuma ya safari hizo ndefu kuna simulizi za madereva wanaodai kukabiliana na changamoto za usalama, mazingira magumu ya kazi na hofu wanapokuwa wakisafirisha kemikali hiyo kwa maelfu ya kilomita.
Kwa madereva wanaosafiri zaidi ya kilomita 2,000 kutoka Dar es Salaam hadi migodi ya Zambia na DRC, kila safari huja na changamoto zake; kuanzia masuala ya usalama, muda mrefu wa kukaa barabarani hadi mazingira ya kazi wanayodai kuwa si rafiki kwa afya zao.
Baadhi yao wanasema hulazimika kuishi ndani ya malori yaliyobeba sulphur kwa wiki kadhaa wakati wa safari hizo, huku wakidai kuwa, wakati mwingine hawapati vifaa vya kutosha vya kujikinga.
Hali hiyo, wanaeleza, imekuwa ikiongeza hofu kuhusu madhara yanayoweza kujitokeza kwa afya na usalama wao.
Baadhi ya madereva wanaeleza kuwa, taarifa za matukio ya vifo vya wenzao walizosikia zimeongeza hofu miongoni mwao wanapokuwa safarini.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, athari za kemikali ya sulphur kwa afya ya binadamu, hususan kwenye mfumo wa upumuaji, zinahitaji uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini kiwango cha madhara yanayoweza kujitokeza, wakieleza kuwa tathmini hiyo inapaswa kuzingatia uchunguzi wa maabara.
Hata hivyo, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inaeleza kuwa sulphur katika hali yake ya kawaida ni kemikali yenye sumu, lakini hatari kubwa zaidi hujitokeza pale inapowaka moto na kuzalisha gesi ya sulphur dioxide, ambayo inaweza kuwa na madhara kwa afya.
Dereva Kassim Jumbe, miongoni mwa wanaosafirisha kemikali hiyo, anasema sulphur husafirishwa kwa kutumia malori aina ya semi-trailer au flatbed, ambayo yana sehemu ya wazi ya kubebea mizigo.
Anasema kabla ya kupangwa mifuko ya sulphur ndani ya lori, huwekwa kichanja maalumu cha mbao au plastiki ili kuzuia mifuko hiyo kugusana moja kwa moja na sakafu ya chuma ya gari.
"Baada ya hapo mifuko hupangwa juu yake na kufunikwa kwa turubai kabla ya safari kuanza," anasema Jumbe.
Pia, anasema malori huwekewa alama maalumu za tahadhari zinazoonesha kuwa yamebeba kemikali hiyo.
Jumbe anasema changamoto huanza kujitokeza safari inapoendelea, hasa kutokana na umbali mrefu unaopita katika njia ya Tanzania, Zambia hadi DRC.
Anasema mikanda inayoshikilia mzigo hulazimika kukaguliwa mara kwa mara ili kuhakikisha haijalegea.
"Mikanda ikilegea unaweza kupoteza mzigo au ukakuta umehamia upande mmoja. Tunalazimika kusimama kila baada ya umbali fulani kuhakikisha kila kitu kiko sawa," anasema Jumbe.
Lakini, anasema changamoto kubwa zaidi si namna ya kufunga mzigo, bali mazingira wanayofanyia kazi bila vifaa vya kutosha vya kujikinga.
Jumbe anasemakampuni nyingi hazitoi vifaa hivyo, hali inayowaacha baadhi ya madereva wakifanya kazi katika mazingira wanayoyaona kuwa hatarishi.
Akikumbuka moja ya safari zake Zambia, Jumbe anasema aliwahi kushuhudia ajali ya malori mawili yaliyokuwa yamebeba sulphur.
Anasema eneo lote ambalo kemikali hiyo ilimwagika lilifungwa utepe na wataalamu waliovaa mavazi maalumu ya kujikinga na harufu ya sulphur kabla ya kuanza kushughulikia tukio hilo.
"Tuliona walivyolichukulia tukio lile kwa umakini mkubwa. Watu wa kawaida hawakuruhusiwa kusogea karibu hadi eneo lilipokuwa salama," anasema.
Kwa upande wa Tanzania, anasema amewahi kushuhudia sulphur ikimwagika barabarani huku wananchi wakisogea karibu bila kufahamu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa.
Dereva Jackson Jalamba anasema changamoto kubwa si namna sulphur inavyosafirishwa, bali kiwango cha maandalizi ya usalama kwa wanaobeba mzigo huo.
Anasema mara nyingi madereva hukabidhiwa magari na kuanza safari bila kupewa vifaa vya kutosha vya kujikinga, licha ya kutumia muda mrefu kuisafirisha kemikali hiyo.
"Madhara ya sulphur huwezi kuyakwepa ukiwa kwenye kazi hii, lakini unaweza kupunguza hatari kama utapewa vifaa sahihi vya kujikinga. Tatizo ni kwamba si kila mwajiri anafanya hivyo," anasema.
Kwa nini wanakubali kuendesha magari?
Jalamba anasema madereva wengi hukubali safari hizo kwa sababu malipo yake ni makubwa kuliko safari nyingine, ingawa wanaamini hayalingani na mazingira wanayokutana nayo njiani.
Akitoa mfano wa safari kutoka Dar es Salaam hadi migodi ya DRC, Jalamba anasema inaweza kuchukua wiki kadhaa kutokana na umbali, foleni mipakani na kusubiri kupakua mizigo.
"Wakati mwingine unafika mgodini unakaa siku tatu, nne au hata wiki nzima unasubiri kupakua. Muda wote unaishi ndani ya gari ambalo limebeba sulphur," anasema.
Nathaniel Jerome anasema hofu kubwa waliyonayo ni kuvuta hewa inayoweza kuwa na madhara.
Jerome anadai kuwa, baadhi ya madereva hupata maumivu ya kichwa, changamoto za mfumo wa hewa na mabadiliko kwenye ngozi, hali wanayohusisha na mazingira ya kazi.
"Kuna mwaka tulisikia baadhi yetu wamekutwa wamekufa kwenye gari. Tukaingia hofu ya usalama, lakini tunashindwa kuacha kwa sababu ukiendesha lori la sulphur unalipwa vizuri kuliko mengine," anasema Jerome.
Anasema baadhi ya kampuni hulipa kati ya Sh2 milioni na Sh3 milioni kwa safari moja, wakati safari nyingine za kawaida hulipa kati ya Sh1 milioni na Sh1.5 milioni.
Kauli kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Maabara wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo, alipozungumza na Mwananchi alisema baadhi ya hofu hizo zinapaswa kutazamwa kwa kuzingatia uelewa wa kisayansi kuhusu kemikali hiyo.
Anasema sulphur katika hali yake ya kawaida ni kemikali yenye sumu.
Ndiyo anaeleza kuwa, hatari kubwa hujitokeza pale kemikali hiyo inapowaka moto na kuzalisha gesi ya sulphur dioxide, ambayo inaweza kuhatarisha afya ya mtu anayeivuta kwa kiwango kikubwa.
"Sulphur haiwaki yenyewe. Inahitaji chanzo cha moto, kama ilivyo petroli au mafuta ya taa," anasema Ndiyo.
Anasema ajali nyingi zinazohusisha sulphur ni za malori kupinduka au mzigo kumwagika bila kuwaka moto.
Akikumbusha matukio yaliyowahi kutokea nchini, anataja ajali ya treni ya Tazara iliyotokea eneo la Pugu pamoja na ajali ya lori karibu na Bwawa la Mindu mkoani Morogoro.
Anasema tahadhari maalumu zilichukuliwa ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kwa mazingira.
Anasema chembechembe za sulphur zinaweza kusababisha muwasho wa macho, ngozi au athari kwa watu wenye mzio, lakini madhara hayo huwa ya muda.
Ndiyo, sheria zinataka kila lori linalobeba sulphur liwe na mpango wa dharura, huku dereva akitakiwa kujua kemikali anayobeba, madhara yake na hatua za kuchukua endapo ajali itatokea.
Kuhusu vifaa vya kujikinga, Ndiyo anasema vinapaswa kutumika wakati wa kushughulikia kemikali hiyo, hasa inapomwagika au wakati wa dharura na si lazima muda wote wa safari.
Wataalamu wa afya wanena
Akizungumza na Mwananchi, Ijumaa Julai 17, 2026 Dk Elisha Osati, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji, alisema suala la madhara ya sulphur linahitaji kuhusisha wataalamu wa maabara wenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa kina na kutoa majibu sahihi ya kisayansi.
“Kwa upande wa madhara ya sulphur, hili ni suala linaloweza kuzungumziwa vizuri zaidi na wataalamu wa maabara wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa sababu wao ndio wenye uwezo wa kufanya uchambuzi wa kemikali hiyo na kubaini athari zake,” alisema.
Daktari Ngozi Hospitali ya Taifa Muhimbili, Magreth Dennis anasema madhara ya sulphur hutegemea mwitikio wa mwili wa mtu.
Anasema si kila mtu anayegusa sulphur hupata madhara kwenye ngozi, akieleza kuwa athari zake hutegemea mwitikio wa mwili wa mtu binafsi dhidi ya kemikali hiyo.
"Mtu ambaye mwili wake una mwitikio wa mzio (aleji) anaweza kupata matatizo ya ngozi baada ya kuigusa, huku mtu ambaye hana mwitikio huo akiwa na uwezekano wa kutopata madhara," anasema.
Akizungumzia hali inayoweza kutokea endapo sulphur inayosafirishwa kwa malori itamwagika katika maeneo ya makazi na wananchi wakaigusa au kuisogelea, Dk Magreth anasema madhara hayo hayawezi kuwa ya kila mtu, bali hutegemea maumbile na uwezo wa mwili wa mhusika kuitikia kemikali hiyo.
"Ili mtu apate madhara, ni lazima mwili wake uwe na mwitikio dhidi ya sulphur akilinganisha hali hiyo na watu wanaopata mzio kutokana na matumizi ya dawa fulani," anasema.
Wamiliki wa malori watetea utaratibu uliopo
Kwa upande wao, viongozi wa vyama vya wamiliki wa malori wanasema usafirishaji wa sulphur unasimamiwa kwa utaratibu maalumu unaojumuisha mafunzo, vyeti na vibali.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa), Issa John anasema Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali huwapa madereva na wasafirishaji mafunzo ya usalama pamoja na vibali vinavyowawezesha kusafirisha kemikali hizo.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Rahim Dossa anasema madereva wanaosafirisha sulphur hupatiwa mafunzo na kuelekezwa namna ya kufuata miongozo ya usalama wakati wa kazi.
NEMC yasisitiza tahadhari
Meneja wa Uzingatiaji wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Hamadi Taimuri anasema ajali yoyote inayohusisha sulphur au kemikali nyingine inapaswa kuripotiwa mara moja kwa mamlaka husika ili hatua za haraka zichukuliwe.
"Si sulphur pekee, bali kemikali yoyote inapobebwa bila kufuata taratibu inaweza kusababisha madhara, ikiwamo uchafuzi wa mazingira," anasema Taimuri.
Anasema sheria zinazitaka kampuni zinazobeba kemikali kuhakikisha zinazingatia masharti yote ya usalama, huku gharama za kusafisha na kurejesha mazingira baada ya ajali zikibaki kuwa jukumu la mhusika.
Hata hivyo, licha ya maelezo ya wataalamu na wamiliki wa malori kuhusu uwepo wa mifumo ya usalama, simulizi za baadhi ya madereva zinaonyesha kuwa bado kuna pengo kati ya taratibu zinazopaswa kufuatwa na hali wanazodai kukutana nazo wakiwa barabarani.