UCHAMBUZI: Magufuli angalia vizuri salfa
Muktasari:
Kamati hizo zimekuja na majibu ya hadidu za rejea yaliyoonyesha kuibiwa mabilioni ya shilingi katika sekta ya madini kutokana na uzembe uliofanywa na viongozi mbalimbali. Tunasubiri hoja za utetezi wa upande wa pili katika sakata hili.
Wasomi wanasema utafiti unapingwa kwa utafiti. Kwa mantinki hiyo ni vigumu kupinga upande uliojitokeza kupitia utafiti bila kufanya mwingine, na hivyo busara inatuelekeza kukubaliana na ripoti za kamati za mchanga wa madini.
Kamati hizo zimekuja na majibu ya hadidu za rejea yaliyoonyesha kuibiwa mabilioni ya shilingi katika sekta ya madini kutokana na uzembe uliofanywa na viongozi mbalimbali. Tunasubiri hoja za utetezi wa upande wa pili katika sakata hili.
Hii ilikuwa ya pili, tayari matokeo ya kamati ya kwanza kuhusu mchanga huo yamendoka na ‘kichwa’ cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuvunjwa bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMMA) na kusimamishwa kazi mkurugenzi wa wakala huo. Uamuzi huo uliibua mshtuko na hofu ya kuyumbisha uwekezaji wa kigeni.
Taarifa za kamati zote mbili zimeibua mapendekezo ambayo bahati nzuri Rais John Magufuli ameyakubali. Mapendekezo hayo yamebainisha maeneo mbambali ambayo yalikuwa ni mianya ya kupotea kwa mapato yatokanayo na madini, hasa katika mfumo wetu wa sheria na mikataba. Maeneo haya yakifanyiwa kazi kwa haraka yanaweza kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya madini na uchumi wa nchi kwa ujumla, ingawa madini yanazidi kupungua nchini.
Pamoja na ripoti hizo kwa ujumla wake, ningependa kuzungumzia hii ya pili iliyowasilishwa na Profesa Nehemiah Osolo juzi, hasa kuhusu kiwango cha sulphur na hasara yake. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuna kiwango kikubwa cha sulphur kilichokuwa kinapotea kwenye kila kontena sawa na wastani wa kilo 7,800. Tangu mwaka 1998 hadi Machi mwaka huu, tani 478,296 za sulphur, zenye thamani ya Sh411 bilioni zilisafirishwa kupitia makontena 61,320 bila kuingiza chochote nchini.
Niliwahi kufuatilia suala hilo hapo nyuma na kubaini kuwa madini hayo ambayo hutumika kutengenezea kemikali ya sulphur, yalikuwa hayafuatiliwi na mtu yeyote na yalikuwa yanawanufaisha hao wafanyabiashara lakini nchi haiambulii chochote.
Katika uchunguzi wangu nilitaarifiwa na maofisa wa TMAA kwamba madini hayo ya sulphur ni kweli hayalipiwi kodi na yanabakia kwenye mchanga kwa sababu teknolojia ya kuyaondoa ni kubwa kuliko thamani ya kiwango cha madini yaliyomo. Hata hivyo, tofauti na maelezo hayo, juzi watalaamu hao wameshuhudia kamati ya Profesa Osoro ikionyesha kuwa katika tani 478,296 tungepata Sh411 bilioni ambazo zimepotelea huko.
Hivi ni kweli TMAA walikuwa wanataka kutuaminisha kwamba hakuna haja ya kuchukua mapato ya madini haya? Hii inatoa tafsiri kwamba, viongozi wengi wanafanya kazi kwa mazoea. Hawaamini kama mabadiliko yanaweza kufanyika wakati wowote. Licha ya juhudi alizozifanya Waziri Muhongo, bado kulikuwa na umuhimu wa yeye kuonyesha uzalendo wake katika sakata hili la mchanga.
Rais hakuwa na sababu ya kutumia gharama na muda kuunda kamati hizo mbili kufuatilia sakata hilo wakati mamlaka na wizara husika ipo.
Kutokana na mazingira hayo, mambo mawili yanayoweza kumsaidia Rais katika harakati hizi, ni kwamba kwa kuwa ameshapiga marufuku shughuli za usafirishaji wake, ni muhimu kuanza maandalizi ya awali kwa nchi kusimika kinu cha uchenjuaji nchini ili kuhakikisha kila aina ya madini yanakuwa na faida kwa Watanzania.
Kama tungekuwa na mashine hiyo hapa nchini, tungeliweza kuchenjua sulphur hiyo na tungetengezea kemikali ambayo ingeweza kusaidia katika maabara zetu za hapa nchini.
Pili, Rais akutane na vijana baadhi wazalendo waliopo katika ofisi za TMAA, wenye taarifa nyingi na zenye ukweli wa kukusaidia katika kuibua madudu mengi zaidi ya taarifa zilizotolewa na kamati hizo mbili.
Mwandishi anapatikana kwa 0716186074