Prime
WHO yafichua ukubwa wa janga la saratani duniani, nyingi zinazuilika
Muktasari:
- Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa tahadhari kuhusu kuongezeka kwa wagonjwa wa saratani duniani, huku likibainisha kuwa zaidi ya watu 26,000 hupoteza maisha kila siku kutokana na ugonjwa huo.
Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa tahadhari kuhusu kuongezeka kwa wagonjwa wa saratani duniani, huku likibainisha kuwa zaidi ya watu 26,000 hupoteza maisha kila siku kutokana na ugonjwa huo na idadi ya wagonjwa wapya inatarajiwa kufikia milioni 35 ifikapo mwaka 2050 endapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Hayo yameelezwa katika Ripoti ya Hali ya Saratani Duniani 2026, iliyotolewa hivi karibuni na WHO kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC), ikionesha kuwa kwa sasa dunia inarekodi wastani wa wagonjwa wapya milioni 20.6 na karibu vifo milioni 10 kila mwaka.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa saratani ndiyo chanzo cha pili kikubwa cha vifo duniani baada ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, huku ikisisitiza kuwa mwelekeo huo unaweza kubadilishwa ikiwa nchi zitawekeza zaidi katika kinga, uchunguzi wa mapema na matibabu yanayowafikia wananchi wote.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, aliyenukuliwa katika taarifa ya shirika hilo, tofauti kubwa zilizopo katika upatikanaji wa huduma za saratani kati ya mataifa tajiri na maskini zinaendelea kugharimu maisha ya mamilioni ya watu.
Tofauti kubwa za huduma
Ripoti inaonesha kuwa wanawake wenye saratani ya matiti katika nchi zenye kipato cha juu wana nafasi kubwa zaidi ya kuishi baada ya kugundulika na ugonjwa huo kuliko wale wa nchi maskini.
Aidha, chini ya theluthi moja ya nchi duniani zimejumuisha huduma za saratani katika mfumo wa huduma za afya kwa wote (Universal Health Coverage), hali inayowaacha mamilioni ya wagonjwa bila matibabu wanayohitaji.
Athari zaidi ya afya
Mbali na kusababisha vifo, WHO imeeleza kuwa saratani ni miongoni mwa magonjwa yanayoacha athari kubwa kwa uchumi wa kaya na ustawi wa jamii.
Kwa mujibu wa utafiti wa kwanza wa shirika hilo uliowahusisha watu wanaoishi na saratani, asilimia 45 ya wagonjwa hukumbwa na changamoto za kiuchumi kutokana na gharama za matibabu na kupoteza kipato.
Saratani zinazoua zaidi
Saratani ya mapafu imeendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo vinavyotokana na saratani duniani.
Kwa wanaume, saratani za mapafu, tezi dume na utumbo mpana ndizo zinazoongoza kwa wingi wa wagonjwa, wakati kwa wanawake saratani za matiti, mapafu na utumbo mpana ndizo zinazoathiri zaidi.
WHO pia imebaini kuwa karibu wagonjwa wanne kati ya 10 wa saratani wanatokana na vihatarishi vinavyoweza kuzuilika.
Miongoni mwa sababu hizo ni matumizi ya tumbaku na pombe, maambukizi ya virusi vya HPV na homa ya ini aina B na C, bakteria wa Helicobacter pylori, unene uliopitiliza, kutofanya mazoezi na ulaji usiozingatia lishe bora.
WHO yatoa mapendekezo
Katika ripoti hiyo, WHO imezitaka Serikali duniani kuunganisha huduma za saratani katika mifumo ya huduma za afya kwa wote, kuongeza uwekezaji katika wataalamu na miundombinu ya afya, kuimarisha kinga ya jamii dhidi ya vihatarishi vya saratani na kuhakikisha wagonjwa pamoja na familia zao wanapata huduma za kijamii na kifedha.
Shirika hilo limesema hatua zitakazochukuliwa sasa ndizo zitakazoamua ukubwa wa mzigo wa saratani kwa vizazi vijavyo, likisisitiza kuwa huduma zinazomweka mgonjwa katikati ndizo zitakazosaidia kupunguza vifo na kuboresha maisha ya watu duniani.
Hali ilivyo nchini
Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania inakadiriwa kurekodi karibu wagonjwa wapya wa saratani 45,000 kila mwaka, huku vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vikiwa takribani 30,000.
Aidha, takribani wagonjwa 27,000, sawa na asilimia 60 ya wagonjwa wapya wa saratani, huhitaji huduma za tiba kwa mionzi, lakini ni wagonjwa 4,000 pekee, sawa na asilimia 15, wanaopata huduma hizo, hali inayoacha idadi kubwa ya wananchi bila huduma kamilifu za matibabu.
Nini kifanyike
Akizungumza na Mwananchi, Daktari Bingwa wa Saratani, Dk Irene Nguma, amesema sehemu kubwa ya wagonjwa wa saratani inaweza kuzuilika kupitia mtindo bora wa maisha na uchunguzi wa mapema.
Ametaja matumizi ya pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara, uzito uliopitiliza na ngono zembe inayoweza kusababisha maambukizi yanayohusishwa na baadhi ya saratani kuwa miongoni mwa vihatarishi vikuu.
Ameshauri wananchi kufanya mazoezi mara kwa mara, kula lishe bora yenye mboga za majani na matunda kwa wingi, kupunguza vyakula vyenye mafuta mengi ya wanyama na vile vilivyosindikwa kupita kiasi, pamoja na kufanya uchunguzi wa afya angalau mara moja au mbili kwa mwaka hata bila kuwa na dalili za ugonjwa.
Dk Nguma amesema uchunguzi wa mapema huongeza uwezekano wa kugundua saratani katika hatua za awali na kuboresha matokeo ya matibabu.
Pia amesema baadhi ya saratani zinaweza kuzuilika kwa chanjo, ikiwemo chanjo ya Hepatitis B inayopunguza hatari ya saratani ya ini na chanjo ya HPV inayokinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutoa chanjo ya HPV bila malipo kwa wasichana wenye umri wa miaka tisa hadi 14 katika vituo vya afya vya umma, huku akiwataka wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hiyo kwa wakati ili kupunguza hatari ya kupata saratani ya mlango wa kizazi baadaye maishani.