Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Saratani ikirudi upya vita yake usipime

Muktasari:

  • Saratani inapojirudia, haileti tu changamoto ya kimatibabu, bali huja na gharama kubwa za kifedha, mtikisiko mkubwa wa kisaikolojia kwa mgonjwa na familia.

Dar es Salaam. ​Wakati takwimu za afya nchini zikionesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani hufika hospitalini ugonjwa ukiwa tayari umesambaa na kufikia hatua ya tatu na nne, kuna upande wa pili wa sarafu hii wenye simulizi za maumivu makali zaidi.

​Hii ni simulizi inayowahusu wagonjwa waliopita kwenye tanuru la matibabu, wakapewa matumaini mapya, na kurejea kwenye familia zao wakiamini wameushinda ugonjwa huo tishio. 

Hata hivyo, wakiwa katikati ya shangwe za ushindi, ghafla hukumbana na hukumu ambayo hakuna mwanadamu anayetamani kuisikia tena maishani mwake: "Saratani imerudi."

​Kwa mujibu wa daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk Emmanuel Nundu, kurejea kwa saratani baada ya matibabu,  ni moja ya changamoto kubwa inayonyemelea wagonjwa wengi.

Anafafanua kuwa hali hii inaweza kujitokeza miezi kadhaa au hata miaka mingi baada ya mgonjwa kumaliza matibabu. 

Hii ndiyo sababu wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa wagonjwa kuendelea kuhudhuria kliniki za ufuatiliaji, hata kama hawahisi dalili zozote za ugonjwa huo.

​"Kliniki hizi za ufuatiliaji si utaratibu wa kawaida tu wa hospitali; ni ngao muhimu ya kiusalama inayosaidia kubaini mabadiliko yoyote mwilini mapema kabla seli za saratani hazijasambaa tena," anasisitiza.


Mtego wa safari ya pili

​Dk Nundu anaongeza kuwa saratani inapojirudia, mara nyingi huja na ukali na changamoto kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzoni.

​Katika baadhi ya wagonjwa, ugonjwa unaweza kurejea katika eneo lilelile ulipoanzia. Hata hivyo, kwa wengine, seli hizo husafiri kupitia mfumo wa damu au limfu na kwenda kushambulia kiungo kingine kabisa cha mwili. 

Hali hii inafanya matibabu kuwa magumu zaidi, huku ikilazimisha madaktari kubadili mbinu za tiba kulingana na hatua mpya ya ugonjwa.

​Uhalisia wa maelezo haya ya kitaalamu unadhihirika wazi unaposikiliza ushuhuda wa wagonjwa waliokubali kufungua kurasa za maisha yao ili kutoa funzo kwa jamii.

​Mwanakheri Mtambalike, mkazi wa Kigogo jijini Dar es Salaam, bado anakumbuka furaha aliyokuwa nayo mwanzoni mwa mwaka 2024.

 Ilikuwa ni baada ya madaktari kumfahamisha kuwa matibabu ya saratani ya nje ya uzazi  aliyokuwa akiyapata, yamezaa matunda kwa kiasi kikubwa.

​Mwanakheri aligundulika kuwa na ugonjwa huo mwaka 2022 na kuanza kliniki ORCI Julai mwaka huo. Baada ya miezi kadhaa ya dozi, afya yake iliimarika na akarejea kwenye majukumu yake ya kila siku.

​"Niliona maisha yamerudi. Nilikuwa na amani nikiamini safari ya saratani imekwisha," anasema Mwanakheri huku akivuta kumbukumbu.


​Gharama ya kupuuza kliniki 

​Hata hivyo, matumaini ya Mwanakheri yalikuwa ya msimu. Anasema madaktari walimpa ratiba ya kuhudhuria kliniki kila baada ya miezi mitatu ili kufuatilia mwenendo wa afya yake, lakini akaiacha ratiba hiyo ipotee hewani.

​Baada ya kurejea nyumbani kwao Ikwiriri, Rufiji mkoani Pwani, umbali wa safari pamoja na hisia za kudhani amepona kabisa, vilimfanya aone hakuna umuhimu wa kurudi hospitalini.

​"Nilikuwa najisikia vizuri kabisa. Nikaona hakuna haja ya kupoteza nauli na muda kwenda kliniki kila baada ya miezi mitatu. Umbali nao ulinikatisha tamaa," anasimulia kwa sauti iliyojaa majonzi.

Machi 2025, ghafla alianza kuhisi dalili ngeni mwilini mwake. Aliporejea Ocean Road kwa uchunguzi wa dharura, majibu yalimvua nguo. Safari hii, maadui wale (seli za saratani) walikuwa wamejichimbia kwenye ini, na tayari ugonjwa ulikuwa umefikia hatua za mwisho.

​Tangu wakati huo, afya ya Mwanakheri imekuwa ikiporomoka kwa kasi. Hadi kufikia Machi 2026, amewekwa chini ya uangalizi maalum akisaidiwa tu kupunguza maumivu makali, kwani matibabu ya chemotherapy na mionzi yamesitishwa, kwa sababu mwili wake hauwezi tena kustahimili vishindo vya tiba hizo.

​"Kama ningejua umuhimu wa kuendelea na kliniki, labda leo hali yangu isingekuwa hivi," anasema huku akishindwa kuzuia machozi.


​Kutoka matiti hadi kwenye tezi

​Kisa cha Mwanakheri kinafanana kwa ukaribu na kile cha Cleopatra Mussa, mkulima wa mpunga na mkazi wa Dakawa mkoani Morogoro.

​Cleopatra aligundulika kuwa na saratani ya matiti mwaka 2019. Baada ya mapambano makali ya matibabu yaliyodumu hadi mwaka 2021, alihitimu dozi na kurudi shambani kwake akiwa na matumaini mapya ya maisha.

​Lakini mwaka 2024, dhoruba ilirejea. Uchunguzi wa kidaktari ulibaini kuwa saratani imerejea tena, na safari hii ikiwa imesambaa kwenye tezi za limfu kuelekea eneo la kwapa. Hali hii imemlazimu kuanza upya safari nyingine ya mateso ya matibabu.

​"Nilidhani nimeimaliza kabisa saratani. Sikutegemea hata kidogo kwamba ingeweza kurudi tena baada ya miaka yote hiyo," anasema Cleopatra, ambaye kwa sasa anaendelea kupambana huku akisali kuwa safari hii atafanikiwa kuudhibiti ugonjwa huo.

​​Uzoefu wa wagonjwa hawa na maelezo ya wataalamu yanatoa somo kubwa kwa jamii.

 Saratani inapojirudia, haileti tu changamoto ya kimatibabu, bali huja na gharama kubwa za kifedha, mtikisiko mkubwa wa kisaikolojia kwa mgonjwa na familia, na kupungua kwa machaguo ya tiba kutokana na mwili kuchoka.

​Wataalamu wanatoa ujumbe mzito katika vita dhidi ya saratani. Kuambiwa "umepona" au "seli hazionekani" si mwisho wa safari. 

Ni mwanzo wa awamu nyingine muhimu ya uangalizi na ulinzi wa maisha yako. Kuzingatia kliniki za ufuatiliaji na kutopuuzia dalili yoyote mpya, ndiyo siri pekee ya kusalia salama.