Sababu wagonjwa wengi kuchelewa matibabu ya saratani
Muktasari:
- Idadi ya wagonjwa wa saratani nchini inaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, huku zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wanaofika katika taasisi hiyo wakigundulika kuwa tayari wako katika hatua za tatu na nne za ugonjwa huo.
Dar es Salaam. Kila siku mamia ya watu hupita kwenye lango la Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) jijini Dar es Salaam, wakibeba matumaini ya kupata majibu ya afya zao.
Wengine huingia wakiwa na hofu, wengine wakiwa na maumivu makali, na wengine wakiwa tayari wamezunguka hospitali kadhaa wakitafuta kilichokuwa kinawasumbua.
Lakini nyuma ya nyuso hizo kuna ukweli unaoumiza.Kwa mujibu wa Meneja wa Epidemiolojia na Takwimu wa ORCI, Dk Johnson Katanga, idadi ya wagonjwa wa saratani nchini inaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, huku zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wanaofika katika taasisi hiyo wakigundulika kuwa tayari wako katika hatua za tatu na nne za ugonjwa huo.
Ni hatua ambazo wataalamu wa afya huzitaja kuwa ni za juu zaidi za maendeleo ya saratani.
"Idadi ya wagonjwa inaongezeka kila mwaka, na zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wanaofika kwetu huwa tayari wako kwenye hatua ya tatu au ya nne ya ugonjwa," anasema Dk. Katanga.
Takwimu hizo zinaibua maswali mengi. Kwa nini Watanzania wengi wanagundua saratani wakiwa wamechelewa? Kwa nini ugonjwa huo unaendelea kukua kimya kimya hadi kufikia hatua za hatari kabla ya wagonjwa kufika kwa wataalamu?
Kwa mujibu wa taarifa za ORCI, wastani wa wagonjwa kati ya 4,500 hadi 5,000 hupokelewa katika taasisi hiyo kwa mwezi kwa ajili ya huduma mbalimbali zinazohusiana na saratani.
Aina za saratani zinazoongoza kwa wagonjwa wengi ni saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya matiti, saratani ya koo, saratani ya utumbo na saratani ya tezi dume.
Wanawake ndio wanaounda takribani asilimia 70 ya wagonjwa wote wanaofika kupata huduma.
"Niliogopa kuambiwa nina saratani"
Lakini nyuma ya takwimu hizo kuna simulizi za watu halisi, ambao leo wanajutia kuchelewa kuchukua hatua.
Rehema Mohamed Chande kutoka Zanzibar ni mmoja wa wagonjwa niliokutana nao katika viwanja vya Ocean Road akiwa anasubiria majibu ya uchunguzi wa saratani alioufanya kupitia vipimo vya CT SCAN na kipimo maalum cha BIOPSY kinachohusisha kuchukua sehemu ndogo ya tishu au seli kutoka sehemu ya mwili inayoshukiwa kuwa na ugonjwa, kisha kuzipeleka maabara ili zichunguzwe kwa darubini na mtaalamu wa magonjwa.
Anasema kwa muda mrefu alikuwa akisikia simulizi za kutisha kuhusu ugonjwa wa saratani, kiasi kwamba hakutaka hata kufikiria kwenda kufanyiwa uchunguzi.
"Nilikuwa nasikia watu wakisema saratani haina tiba. Wengine walikuwa wakisema ukianza matibabu ndiyo unakufa haraka zaidi. Hizo kauli zilinifanya niogope sana kwenda kupima," anasimulia kwa huzuni.
Kwa miezi kadhaa aliendelea kuvumilia dalili zilizokuwa zikijitokeza mwilini mwake akiamini huenda zingepotea zenyewe.
Lakini hali ilipozidi kuwa mbaya ndipo alipoamua kutafuta msaada wa kitabibu.
Rehema anakiri kuwa kama angefanya uchunguzi mapema, huenda safari yake ya matibabu isingekuwa ngumu kama ilivyo sasa.
"Nilikuwa naambiwa ni homa ya kawaida"
Kwa upande wake, Stumai Mkumba kutoka Kutoka Kiberege Morogoro anasema kilichomchelewesha zaidi ni majibu aliyokuwa akipewa katika baadhi ya vituo vya afya alivyovitembelea mwanzoni.
Anasema mara kadhaa aliambiwa tatizo lake halikuwa kubwa na kupewa dawa za maumivu pamoja na matibabu ya magonjwa ya kawaida.
"Nilikuwa nikisumbuliwa na tatizo la kuwashwa sehemu za siri, nilikuwa nikijikuna na kupata maumivu makali hasa nyakati za usiku nilikuwa nikiambiwa ni maradhi ya fangasi na hospitali zingine niliambiwa nina UTI sugu nikawa ninapewa dawa za maumivu na kurudi nyumbani. Dalili zilipoendelea ndipo baadaye nikafikishwa kwa wataalamu zaidi hapa Ocean Road," anasema.
Anasema muda ulipotea huku ugonjwa ukiendelea kukua bila yeye kujua.Simulizi yake inaakisi changamoto inayowakumba wagonjwa wengi ambao dalili zao huweza kufanana na magonjwa mengine katika hatua za awali.
Imani potofu zinaua kimya kimya
Kwa mujibu wa Dk Katanga, sababu za wagonjwa wengi kufika hospitalini wakiwa wamechelewa ni pamoja na uelewa mdogo kuhusu ugonjwa wa saratani, imani potofu zilizojengeka katika jamii pamoja na kuchelewa kutafuta huduma za kitaalamu.
Wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza kuwa saratani nyingi zinaweza kutibika au kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa iwapo zitagunduliwa mapema.
Hata hivyo, bado wananchi wengi huanza kujitibu kwa tiba mbadala, maombi pekee, au kusubiri dalili ziondoke zenyewe kabla ya kwenda hospitali. Katika kipindi hicho, ugonjwa huwa unaendelea kukua kimya kimya.
Kila mgonjwa anayegundulika akiwa katika hatua za mwanzo, huwa na nafasi kubwa zaidi ya kufaidika na matibabu kuliko anayefika akiwa katika hatua za mwisho.
Ndiyo maana wataalamu wanaeleza kuwa vita dhidi ya saratani si vita vya dawa pekee, bali pia ni vita vya muda.
Kadiri mgonjwa anavyochelewa kufanya uchunguzi, ndivyo nafasi ya ugonjwa kusambaa mwilini inavyoongezeka.
Na wakati takwimu zikionyesha wagonjwa wanaongezeka mwaka hadi mwaka, ujumbe unaotolewa na wataalamu unabaki kuwa mmoja: wananchi wajenge utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kutopuuzia dalili zinazojitokeza mwilini.
Kwa sababu katika mapambano dhidi ya saratani, siku moja inayopotea leo inaweza kuwa tofauti kati ya matumaini ya kupona na safari ngumu ya kupambana na ugonjwa uliokwisha kusonga mbele.
Na kwa zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wanaofika Ocean Road wakiwa tayari katika hatua za tatu na nne za saratani, swali linalobaki ni moja: Je, Watanzania wataanza lini kuichunguza saratani kabla haijawahi kuwafikia?
Wakati takwimu zikionyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani hufika hospitalini ugonjwa ukiwa tayari umefikia hatua za tatu na nne, simulizi inayofuata itafungua ukurasa mwingine wa maumivu ambao wengi hawaujui.
Ni simulizi za wagonjwa waliopambana, wakapokea matibabu, wakaambiwa wameushinda ugonjwa na kurejea katika maisha yao ya kawaida, lakini baadaye wakakumbana na mshangao wa saratani kurejea tena kwa kasi na nguvu zaidi.