Madhara 10 kutumia P2

Madhara 10 kutumia P2

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya wametaja madhara 10 yanayoweza kumpata mwanamke anayetumia dawa za dharura za kuzuia ujauzito ‘Emergence Contraceptive Pills’ vidonge maarufu P2 mara kwa mara ikiwemo kutokwa na damu kwenye uke isiyo ya hedhi.

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wametaja madhara 10 yanayoweza kumpata mwanamke anayetumia dawa za dharura za kuzuia ujauzito ‘Emergence Contraceptive Pills’ vidonge maarufu P2 mara kwa mara ikiwemo kutokwa na damu kwenye uke isiyo ya hedhi.

Matumizi ya mara kwa mara yametajwa kuleta shida zaidi na kwamba endapo mtu akitumia kwa kawaida na kufuata ushauri wa daktari haiwezi kupata shida.

Mfamasia na Mkufunzi wa shule ya famasia kutoka Chuo Kikuu Muhimbili (Muhas), David Myemba alitaja madhara hayo na kusema dawa hizo pia zinaweza kuleta madhara madogo ‘side effect’ kama kujisikia kichefuchefu, kichwa kuuma, kizunguzungu na kuharisha.

Alisema matumizi ya dawa ambazo zinamezwa kiholela hasa za kuzuia mimba au zile za kutibu matatizo yanayohusiana na hedhi hutengeneza tatizo.

“Husababisha mabadiliko ya mzunguko wa hedhi kwa wengi, kwa mwezi anaweza kupata mara mbili au hapati kabisa, anawahi sana, anachelewa sana na akipata inakua ni nzito, damu ni nyingi. Inatoka mpaka anapata kizunguzungu au mpaka kupoteza damu nyingi akapata anaemia au damu kidogo tunaita spot mpaka akawa anapata wasiwasi,” alisema.

Myemba alisema akiwa anameza kwa wiki mara mbili au tatu ni sawasawa na mtu anayetumia dawa za uzazi wa mpango zile za kawaida, kwa hiyo madhara yanayoweza kutokea ni kuongezeka uzito kupita kiasi kutokana na homoni anazozizalisha.

“Unaweza ukakuta akapata shida katika mzunguko wa damu, wakati mwingine unakuta damu inatengeneza mabongebonge na kama alikuwa anatumia mara kwa mara inakuwa ni rahisi kupata kiharusi au stroke,” alisema Myemba.

Alitaja madhara mengine kuwa ni shida katika mifupa ambayo huwa dhaifu kutokana na kutumia kwa muda mrefu na mara nyingi mtu huyo akipata ajali ya kawaida huvunjika mifupa kwa haraka ikiwemo mguu au mkono.

Myemba alisema madhara mengine ni kupata magonjwa ya zinaa na virusi vya Ukimwi.

“Huona kitendo cha kutumia kinga unakuwa unakipuuza, mwisho wa siku unaona itakuwa rahisi zaidi kwako kupata magonjwa ya ngono, zinaa kwa kuwa unasema nitafanya bila kinga na kesho yake nitatumia P2, lakini kumbe unajiweka karibu zaidi kupata magonjwa ya zinaa.”

Alitaja madhara mengine kuwa ni kupata mimba zisizotarajiwa kwa kuwa uhakika wa dawa hiyo kufanya kazi ni saa 24 na zinazosalia huwa ni bahati nasibu ingawaje imetajwa ni saa 72.

“Ndani ya saa 24 ufanisi wake ni mkubwa na 72 bado inaweza kufanya kazi, lakini si kama awali kwa hiyo unaweza ukafocus zaidi kuamini dawa mwisho wa siku ukapata dawa ambayo ni feki au umepita muda ukapata ujauzito ambao hukupanga, hapo wengine wataanza kutoa mimba unaongeza madhara,” alisema.

Alitaja madhara mengine ni kuuweka mwili katika matumizi ya dawa kisaikolojia na kiafya, jambo ambalo si zuri.

“Zinaweza kusababisha vipele katika ngozi. Pia vagina bleeding au kutokwa na damu kwenye uke, japo hii haijitokezi mara nyingi.”

“Lakini anaweza kupata shida katika kizazi, hasa kupata saratani katika uzazi, lakini hii ni kama akizidisha matumizi kupita kiasi, ikawa ni sawa na kutumia dawa za uzazi wa mpango.”

Alionya kuwa madhara makubwa zaidi ni pamoja na kushindwa kupata watoto pindi wanapokuwa na uhitaji na wengine kupata mimba ambazo zinatoka mara kwa mara.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dk Jane Muzo alishauri wanawake kuzitumia dawa hizo kwa dharura na si vinginevyo.

“Ni dawa ambayo inabidi kama ukiitumia uchukue tahadhari ili ujizuie usitumie tena kwa sababu wanawake wengi wanalalamika kwamba hedhi zao kidogo zimebadilika, hautakuwa sawa ukitumia mara kwa mara,” alisema Muzo.

Hata hivyo, Baraza la Famasia nchini, limeagiza kuwa P2 ni dawa ya cheti ambayo inaruhusiwa kuuzwa katika famasi mpaka kitolewe cheti cha daktari.