Madhehebu mapya ya Ukristo wa Afrika kuanzishwa

Mwinjilisti,Silvanus Ngemera akionyesha kitabu cha Dini mpya ya ukristo wa Kiafrika kilichoandikwa (African Orthodox Derekh) alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Picha Sunday George
Muktasari:
- Madhehebu yaitwayo African Orthodox Derekh yanalenga kuwatoa Watanzania na Waafrika kwa ujumla katika utamaduni wa kigeni ambao wanaufuata kupitia dini na mahubiri ya fedha yaliyotajwa kutawala hivi sasa.
Dar es Salaam. Wakati dini ikihusishwa na utamaduni wa eneo ilipoanzia, Mwinjilisti Silvanus Ngemera (67) ameanza mchakato kuanzisha madhehebu mapya ya Kikristo yatakayorejesha utamaduni wa Mwafrika.
Madhehebu hayo yatakayoitwa African Orthodox Derekh yanalenga kupambana na mmomonyoko wa maadili, kuachana na dhambi, pamoja na kuuishi utamaduni wa asili ya Mwafrika.
Mwinjilisti Ngemera amesema Waafrika wanapaswa kutambua kuwa, yapo madhehebu yao, ambayo kila mtu mwenye Mungu ndani yake ana uwezo wa kutenda kwenye madhehebu hayo na si watu maalumu kama ilivyozoeleka.
Ameyasema hayo leo Ijumaa ya Septemba 6, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
"Ukristo huu mpya hauna ngazi ndani yake, unamuhusu Mwafrika mwenyewe. Hakutakuwa na mahubiri ya fedha na hatutakuwa na nyimbo wala vyombo vya kizungu kwenye masinagogi yetu, tutakuwa na nyimbo zetu za asili za makabila.
Mwinjilisti Ngemera ambaye ametamba ni mkereketwa wa maendeleo ya Waafrika weusi, amesema anawaona ni watu wa kubaki nyuma katika mambo mengi, hivyo ameamua kuanzisha madhehebu hayo kwa ajili ya kuleta mapinduzi kwao.
Amesema madhehebu hayo ni maalumu kwa Waafrika wote katika nchi 42 Kusini mwa Jangwa la Sahara na katika Sinagogi litakuwa na muundo wa utawala na mabadiliko ya ufundishaji.
"Tutatumia biblia hii hii ya Kiebrania iliyoandikwa lugha ya Kiingereza pamoja na zilizotafsiriwa katika lugha zetu, mfano hapa mimi ninayo biblia ya Kihaya.
"Ukristo ni kuacha dhambi na sisi tutahubiri kujenga Ukristo ndani ya mioyo ya watu na masinagogi yetu yatakuwa na mkuki msalaba ambao ndio alama ya African Orthodox Derekh," amesema.
Ameongeza kwamba Ukristo wa Kiafrika ni ule ulioshikamana na utamaduni chanya wa Mwafrika bila kujumuisha miungu, mizimu, uaguzi, kuloga, uchawi, matambiko, ramli, na dhambi zingine.
"Madhehebu yote ya Ukiristo Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ni matawi ya madhehebu ya Ulaya na Marekani na kwa jinsi hii yanaongozwa kutokea Ulaya na Marekani. Kuongozwa kutokea huko unakuwa ni kama ukoloni wa dini ambao haukukusudiwa na Mungu wala mjumbe wake, Yesu Kristo."
Amesema kutokana na mmeguko mkubwa na utitiri wa madhehebu na makanisa binafsi hapa Afrika, sasa Ukiristo umekuwa kama mzaha. Ni vigumu kujua wakati mwingine kama hicho kinachofanyika kwa jina la ukiristo ni dini, hila, utapeli, biashara, uchawi au laana.
"Ukiristo pia unaonekana kumezwa na fedha na sasa tunahubiri sadaka badala ya kumhubiri Mungu. Tukishafanya uamuzi huu wa kujitenga kiuendeshaji na Ukiristo wa kigeni, tunafundisha Uucha Mungu wa maneno mafupi na vitendo virefu vya imani na haki.
"Ukristo huu unatupa nafasi waamini wote kujihudumia kiroho huku tukiwa ni watumishi wenye nguvu ya kufukuza uchawi na kukemea pepo, sisi wenyewe.
"Vilevile, tunatumia Kiebrania badala ya Kiyunani. Yesu Kristo tunamwita Isho Hamashiach, Maria tunamwita Maryamu, Biblia inaitwa Mikra, Sabato inaitwa Shabbat na kanisa tunaliita sinagogi na Wakiristo wanaitwa Waderekhi au 'Watu wa Njia ya Mungu."