Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madiwani 38 kati ya 44 Lindi waazimia kumng’oa Meya

Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi Frank Magari

Dar es Salaam. Madiwani 38 kati ya 44 wa manispaa ya Lindi wamepiga kura ya kutokuwa na imani na meya wa halmashauri hiyo, Frank Magari wakimtaka ajiuzulu nafasi hiyo kwa madai ya matumizi mabaya ya madaraka.

Hata hivyo, Magari akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi, Septemba 29, 2023 amesema tuhuma hizo sio za kweli, bali zinalenga kumchafua katika nafasi huku akisema kila jambo linalotekelezwa linafuatwa utaratibu.

Katika barua yao walioandika Septemba 26, 2023 kwenda kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Lindi, wakiambatanisha saini zao walidai Magari anatakiwa kujiuzulu kufuatia ukiukwaji wa sheria na kanuni na matumizi mabaya.

Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Juma Mnwele alikiri ofisi yake kupokea taarifa ya kutokuwa na imani na Magari iliyowasilishwa Septemba 26 mwaka huu.

“Hata hivyo, ofisi hii haitaendelea na hatua zozote hadi hapo kifungu cha 5(2) cha kanuni za kudumu za halmashauri ya manispaa ya Lindi za mwaka 2014 zilizotungwa chini ya kifungu 42(1) cha Sheria za Serikali za Mitaa sura 288 zitakapozingatiwa.

“Karatasi ya saini sio sahihi, halafu sahihi zilikuwa la jambo jingine wao wamenyofoa mahala wakabandika huku hivyo wameharibu. Barua haikusainiwa, wala haielezi wanataka nini wamenipa taarifa tu,” alisema Mnwele.

Katika barua hiyo madiwani 34 waliosaini walidai Magari alisaini mkopo wa Sh1.5 bilioni bila idhini ya Baraza la Madiwani, wakisema hatua inakatazwa kwa mujibu wa kanuni za halmashauri ibara ya 45(2)kifungu (f).

Mbali na hilo, madiwani hao, Magari alifanya uamuzi wa kununua matumizi (huduma) upimaji na kulipa fidia eneo la Likong’o, Mto Mkavu na Gezaulole bila ya kupitisha katika Baraza la Madiwani.

“Anakiuka vikao vya halmashauri vya bajeti ya mwaka kwa siku moja badala ya siku mbili kama ibara ya 6 (a) na (b) inayotaka. Pia, kutosimamia kikao cha mkutano wa mwaka na kazi katika baraza la robo ya 4 ya mwaka.

“Kutengua maagizo ya baraza ya robo ya nne ya mwaka 2021/22 lililoagiza taarifa za Mkuhumi na mradi wa upimaji viwanja kiitwe kikao maalumu kijadiliwe badala ya taarifa hizo kufanya kienyeji,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Kwa upande wake, Magari alisema hakuna tuhuma dhidi yake, hata zingekuwepo basi zingeenda kwa wataalamu. Alisema Sh 1.5 bilioni ni mikopo uliotolewa kwa halmashauri zaidi ya tano zikiwemo za Chamwino na Siha.

“Huu sio mkopo wenye riba bali unasaidia kuijenga uwezo halmashauri katika masuala ya upimaji wa miji. Hii barua imeleta mgororo miongoni mwa madiwani ambao hawakujua ishu ya meya.

“Madiwani walijua barua iliyoandikwa ni kwenda kwa mkurugenzi wakitaka ufafanuzi kuhusu masuala hayo. Ndio maana baadhi yao wamegawanyika na kuandika barua za kukana kilichoandikwa na wenzao,” alisema Magari.

Magari amesema ukisoma kwa umakini barua iliyoandikwa haina mwandishi, ndio maana hawajafuata utaratibu unaotakiwa wa kumuandika tuhuma dhidi yake, badala yake wamefanya makosa katika mchakato huo.

 Alisema katika halmashauri yao wamekaa vikao mbalimbali 11 kikiwemo cha mipango miji kilichoketi mara mbili huku akiwashangaa baadhi ya madiwani hao wakisema hawajakaa vikao wala kushirikishwa.

 “Tulikaa kikao cha kamati ya fedha, lakini kinachoidhinisha mambo yote ni kikao cha baraza kilichoketi mara tatu na tulijadili habari ya mradi wanaozungumzia.

 “Mwisho wa siku madiwani hawa waliomba kwenda kutembelea eneo la mradi, usafiri uliandaliwa walikwenda, wakapiga picha na kuweka kwenye mitandao ya kijamii.Nashaanga mradi wanaosema hawaijuhi walikwenda na kupiga picha,” alisema Magari.

 Hata hivyo, lilimtafuta mmoja wa madiwani (jina limehifadhiwa) aliyesaini barua hiyo ambaye aliruka kihunzi akimtaka mwandishi amtafute katibu wao, lakini hakutaka kumtaja akisema ndiyo msema wa suala hilo.