Madiwani Hai wataka mahindi ya msaada yafikishwe vijijini

Muktasari:

  • Madiwani wa Halmshauri ya Hai mkoani Kilimanjaro wameomba kuletewa mahindi ya bei nafuu ili kukabiliana na hali ya njaa inayokabili wananchi

Hai. Madiwani wa Halmashauri ya Hai mkoani Kilimanjaro wameomba kufikishiwa mahindi ya bei nafuu yaliyotolewa na Wakala wa Hifadhi ya Taifa Chakula (NFRA) ili kukabiliana na uhaba wa chakula.

Pia wame mahindi hayo yauzwe katika vipimo vya rejareja ili kuwawezesha wananchi wenye kipato cha chini kumudu kununua bada ya kipimo cha kilo 50 kinachouzwa Sh44, 000.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Januari 26, Madiwani wamesema mahindi hayo yanapatikana kwenye jengo la maktaba peke yake, hivyo kuleta usumbufu kwa wananchi kuchukua muda mrefu kuyapata.

"Tumeshalalamika kwa viongozi husika wakiwamo wa halmashauri mahindi yaletwe kwenye kata zetu ili kuwapunguzia gharama ya kufuata mahindi hayo halmashauri lakini hakuna jibu," amesema.

Diwani wa Kata ya Kia, Tehera Mollel amesema walitangaziwa mahindi hayo yanauzwa kwa bei nafuu kwa wananchi ili kila mtu aweze kupata, lakini yanapatika  kwa kutumia gharama kuyafuata  halmashari jambo ambalo limekuwa kero kwa wananchi.

"Sisi tunapata lawama kutoka kwa wananchi wakitaka huduma hiyo isogezwe karibu ikiwamo ofisi za kijiji, kufuata mahindi huko halmashari ni gharama, ni afadhali kununu hayo ya mtaani hata kama ni ghali," amesema Azizi Simbano ambaye ni Diwani wa Masama Rundugai.

Amesema kwa mtindo wa utoaji wa mahindi hayo unaonekana siyo siyo msaada, kwani bei yake haijarahisishwa.

“Mwananchi anapenda kununua sado mbili au tatu, debe moja na kuendelea kutokana na hali ya maisha ilivyo, hivyo tunaomba chakula hicho kisogezwe karibu na kiuzwa kwa bei nafuu,” amesema.

Hata hivyo, akizungumzia suala hilo, Ofisa Kilimo wilayani humo, David Lekei amesema utaratibu wa kupeleka chakula kwenye kata zao haupo.
“Ni kutokana na suala la ulinzi ambao kwenye hizo kata haupo.

Hata gharama ya kuyasafirisha ni kubwa. Hivyo waendelee na utaratibu wa kukusanya fedha na kumpa Mtendaji na Mwenyekiti wa Kijiji kuyalipia na kuwafikishia kwa wananchi,” amesema.