Madiwani Mbozi wapitisha azimio kutokuwa na imani na mkurugenzi

Muktasari:
- Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wamepitisha azimio la kutokuwa na imani na mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hanji Godigodi kutokana na upotevu wa Sh187 milioni za ushuru wa kahawa.
Songwe. Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wamepitisha azimio la kutokuwa na imani na mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hanji Godigodi kutokana na upotevu wa Sh187 milioni za ushuru wa kahawa.
Pia, wamemtuhumu mkurugenzi huyo kwa kuwadharau madiwani na watumishi walio chini yake sambamba na kuficha taarifa za mapato ya kahawa.
Hayo yameibuka leo Ijumaa Aprili 30, 2021 katika kikao cha baraza la madiwani wakati wakijadili ajenda namba saba ya kikao kilichopita na kuhoji upatikanaji wa Sh750 milioni za ushuru wa kahawa wakati awali ilikisiwa makusanyo ni Sh950 milioni.
Mkurugenzi huyo alitetea kiwango hicho na kudai hakuna watu wanaodaiwa na pia kahawa imeisha viwandani lakini madiwani kupitia kamati ya fedha iliamua kuunda kamati kufuatilia kwenye viwanda na kukuta kahawa ipo.
Diwani wa Ipunga, Barton Sinienga amesema wakati wakifuatilia walikuta kahawa ipo viwandani na walibaini kuna Sh366 milioni hazikuandikiwa maelezo sehemu yoyote na kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh120 milioni zilitakiwa kulipwa na mkulima mmoja mkubwa na Sh187 milioni hazikuwa na maelezo yoyote.
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo amewashauri madiwani hao kufuata sheria na kanuni akitaka wawasilishe hoja zao kwa maandishi ili kutoa nafasi kwa mkuu wa Mkoa kuzisikiliza na kutoa nafasi kwa mtuhumiwa kujibu.
Kwa upande wake Godigodi aliomba kutoa ufafanuzi wa tuhuma alizorushiwa lakini hakupata nafasi ya kufanya hivyo.