Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madiwani wajiunga na Jeshi la Akiba

Diwani wa kata ya Korongoni, Issa Buliro akizungumzia kuhusiana ma kujiunga na Jeshi la Akiba

Muktasari:

  • Madiwani hao wamesema wameamua kujiunga na Jeshi la Akiba wakieleza kuwa hatua hiyo itaimarisha ushirikiano wa  kiusalama kati yao, askari jamii na wananchi katika kata wanazoziongozaa.

Moshi. Zaidi ya madiwani 12 wa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, akiwamo Meya wa Manispaa hiyo, wamejiunga na mafunzo ya Jeshi la Akiba wakisema hatua hiyo inalenga kuimarisha ulinzi na usalama katika kata wanazoziongoza na kuongeza ushiriki wao katika kulinda amani ya taifa.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi kesho Jumanne, Julai 21, 2026 katika Uwanja wa Mashujaa uliopo Manispaa ya Moshi.

Akizungumza leo Julai 20, 2026, Diwani wa Kata ya Msaranga, Ally Dunga amesema uamuzi wa kujiunga na Jeshi la Akiba umetokana na dhamira ya kuchangia utekelezaji wa dhana ya ulinzi wa taifa na kuimarisha ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Lengo letu ni kuongeza nguvu kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. Tunataka pia kuwa sehemu ya utekelezaji wa dhana ya ulinzi wa taifa na kuhakikisha maeneo yetu yanakuwa salama,” amesema Dunga.

Diwani wa kata ya Msaranga, Ally Dunga akizungumzia kujiunga na Jeshi la Akiba

Amesema zaidi ya madiwani 12, wengi wao wakiwa vijana, wamejitokeza kushiriki mafunzo hayo kwa hiari, wakiamini yatawajengea uwezo wa kushirikiana kwa karibu na askari jamii pamoja na wananchi katika kulinda usalama wa kata zao.

“Tutapata uelewa mpana wa masuala ya usalama na kujilinda, jambo litakalotuwezesha kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda maeneo yao,” amesema.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Korongoni Issa Buliro, amesema mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha usalama katika jamii na wakati huohuo kutoa hamasa kwa vijana wengine kujiunga na Jeshi la Akiba.

“Hii ni mara ya kwanza Manispaa ya Moshi kuwa na idadi kubwa ya madiwani vijana. Tunataka kuwa mfano kwa vijana wengine kwa kushiriki katika shughuli za ulinzi wa taifa kupitia Jeshi la Akiba,” amesema Buliro.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawapa uwezo wa kutoa ushauri katika kamati za ulinzi na usalama za kata na mitaa pamoja na kushiriki katika kuhamasisha uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi wa jamii.

Mkazi wa Manispaa ya Moshi, Dastan Rumisha, amepongeza hatua hiyo akisema inaweza kuwa chachu ya kupunguza vitendo vya uhalifu vinavyoripotiwa katika baadhi ya maeneo ya manispaa hiyo.

“Tumekuwa tukishuhudia matukio ya uporaji wa simu na pochi katika baadhi ya maeneo. Ninaamini mafunzo haya yatawawezesha madiwani kushirikiana kwa karibu zaidi na vyombo vya dola na kuongeza usalama wa wananchi,” amesema.

Naye Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo amesema madiwani wameamua kujiunga na Jeshi la Akiba kwa hiari ili kuhamasisha wananchi, hususan vijana, kushiriki katika shughuli za ulinzi wa taifa.

“Jeshi la Akiba limeanzishwa kwa mujibu wa sheria za nchi na kila Mtanzania mwenye sifa anaweza kujiunga. Tunatarajia hatua yetu itakuwa chachu kwa vijana wengine kushiriki katika kulinda amani na usalama wa nchi,” amesema Kidumo.

Kwa upande wake, Kaimu Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Moshi, Richard Kapiki amesema hadi sasa madiwani 12 wamejiandikisha kushiriki mafunzo hayo, ambayo yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Moshi.