Madiwani wataka mradi uondoe migogoro ardhi

Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya wakiwa kwenye kikao cha robo ya kwanza cha kujadili taarifa mbalimbali za maendeleo. Picha na Mary Mwaisenye.

Muktasari:

  • Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya wataka wataalamu kutumia mradi wa uboreshaji usalama wa miliki za ardhi kutatua migogoro iliyo kwenye wilaya.

Chunya. Madiwani wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya, wataka mradi wa uboreshaji usalama wa miliki za ardhi (LTIP), utumike kuhakikisha utatuzi wa migogoro wailayani humo, na hivyo kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

 Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Digital, baadhi ya madiwani hao wamesema migogoro ya ardhi imekuwa ikikwamisha shughuli za maendeleo, na kwamba kutokana na baadhi ya vijiji kutoeleweka wao ni wa eneo gani, kumesababisha wananchi kushindwa kushiriki za shughuli za maendeleo.

Fide Mwalukasa, Diwani Viti Maalumu, amesema mpango huo unaolenga kuwa na matumizi bora ya ardhi, utakuwa suluhu ya migogoro iliyokuwa imedumu kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Diwani Aden Tajack wa Kata ya Nkung'ungu, amesema: “Kata yangu inapakana na Wilaya ya Songwe, kuna migogoro ya mipaka kati ya Kata ya Ngwala iliyopo Songwe na Kata ya Nkung'ungu ambayo iko Chunya,” amesema na kuongeza;

“...kufuatia hilo kuna baadhi ya wananchi, pale unapowaendea juu ya kuchangia maendeleo ya kata, watakwambia wako wilaya ya Songwe, lakini huduma za kijamii kama afya; wanapata kwenye zahanati ya Nkung'ungu.:

Hivyo, diwani huyo ameomba Serikali kupitia mpango huo ambao unasimamiwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, utumike ili kuondoa sintofahamu hiyo katika kata yake na zile jirani zinazopakana na wilaya nyingine.

Akizungumzia hilo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Ramadhani Shumbi ambaye ndiye alikuwa akiongoza kikao hicho cha baraza la madiwani cha robo ya kwanza, amewataka madiwani kuwa sehemu ya utatuzi wa migogoro ya ardhi.

“...shirikianeni na na mabaraza ya ardhi ya vijiji ili kuhakikisha maendeleo hayakwami...migogoro ya vijiji na vijiji ndani ya kata haipaswi kuendelea kwani kila mtu ana haki ya kuishi mahali popote katika nchi... ilimradi havunji sheria...diwani ahakikishe anakuwa sehemu ya utatuzi wa migogoro kwa kuitisha mikutano na kuelimisha wananchi,” ameeleza Shumbi.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji mbele ya baraza la madiwani, Ofisa Mipango Miji wilayani humo, Sunday Mwakalebela, amesema mpango wa matumizi ya ardhi vijijini kupitia LTIP, unalenga kuboresha usalama wa miliki za ardhi kwa wananchi waishio mjini na vijijini, ambapo hati milioni 2.5 zitatolea.

Mwakalebela amesema mpango huo umekusudia kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji na watumiaji wengine pamoja na kuboresha usalama wa miliki za ardhi, ambapo amebainisha kuwa mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi miwili kwenye vijiji vine, ambapo kazi itafanyika siku 14 mpaka 15.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Mayeka akizungumzia hilo amemtaka Mkurugenzi kuhakikisha wataalamu wanafika maeneo yote yenye migogoro, huku wakikutana na wakuu wa wilaya zote zinazopakana na chunya, na hivyo kumaliza mgogoro uliopo.