Sh21 bilioni kujenga barabara Mbeya

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa akizungumza na watendaji wa Serikali wakati akifungua Mkutano wa kutoa taarifa ya kuanza ujenzi wa barabara za ndani zenye urefu wa kilometa 12.3 zenye thamani ya Sh 21 billioni. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Zenye urefu wa kilometa 12.3 ambazo zitajengwa kwa awamu mbili kwa kiwango cha lami hali  itakayopunguza changamoto ya msongamano wa magari kwenye barabara kuu.

Mbeya. Serikali imetoa zaidi ya Sh21 bilioni kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi wa  ujenzi wa barabara za ndani  zenye urefu wa kilometa 12.3 ambao utakamilika kwa kipindi cha miezi 15.

Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa   amesema jana Alhamisi Oktoba 26, 2023 wakati wa mkutano wa kutoa taarifa ya kaunza utekelezaji wa mradi uboreshaji miundombinu ya miji na kuongeza ushindani kwenye uwekezaji kupitia mradi wa Tactic.

Mradi huo ambao utasimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) na kutekelezwa  na Kampuni ya Chonging International Construction Corparation.

“Kimsingi tuishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson kwani mradi huo utaondoa  changamoto kubwa kwenye barabara za mitaa ambazo sasa inakwenda kuondoka na Mbeya kuwa na hadhi ya kuwa Jiji la mfano,”amesema.

Amesema Maendeleo hayo ni kutokana na ufuatiliaji  wa karibu wa Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson sambamba na ushirikina wa madiwani na kufafanua kuwa awali  Septemba 23 mwaka huu walisaini mkataka jijini Dar es Salaam.

“Uwepo wa barabara hizo utapunguza msongamo katika eneo la Kabwe na Uyole na kwamba zitajengwa kwa kiwango cha kimataifa sambamba na  kufugwa taa za kisasa.”

“Jiji la Mbeya linakwenda kuwa na sura mpya licha ya kuwepo na uhitaji wa barabara zenye urefu wa kilometa 400 ambazo tayari Spika wa Bunge na Mbunge ameziombea kwa Rais Samia Suluhu Hassan na tunatarajia tutapokea fedha wakati wowote,”amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema  Mkoa wa Mbeya kwa sasa kumekucha kwa vurugu za kimaendeleo kwa kuboreshwa miundombinu ya barabara na kwamba huo ni upendo wa hali ya juu  wa Serikali ya awamu ya sita.

“Tunaamini wakandarasi waliopewa kazi wako vizuri na niombe mradi huo utekelezwe kulingana na namna mikataba yetu inavyoeleza kwa kwenda kwa kasi ya kipekee,”amesema.

Amesema kitendo cha Serikali kuelekeza miradi ya barabara njia nne kutoka Igawa mpaka Ifisi yenye urefu wa kilometa 29 sambamba na hizi za ndani  zenye urefu wa kilometa 12.3 sambamba na ufungaji wa taa zitafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi,” amesema.

Malisa amewaagiza makandarasi waliopata zabuni kutoa kipaumbele cha ajira na vibarua kwa vijana wazawa sambamba na kudhibiti wizi wa vifaa vya huku akisisitiza Rais Samia atapata maua yake katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Mkuu 2025.

“Niwasihi madiwani waelekezeni wananchi Serikali inafanya nini katika kuboresha utekelezaji wa miradi lengo ni kuona Watanzania wanafanya shughuli zao katika barabara zilizo na ubora na kufungwa taa za kisasa,”amesema.

Mhandisi mkazi wa mradi huo, Jofrey Kanjanja amesema utajengwa kwa miezi 15 kwa barabara za kiwango cha lami sambamba na kuwekwa mifereji yenye ubora ambapo utekelezaji wake utakuwa wa awamu mbili  katika barabara tano.

Ametaja barabara hizo na kilometa kwenye mabano kuwa ni Uyole -Itezi (1.8) Kabwe –Sido (1.200) Ilomba -Machinjioni (3.8), Iziwa (2) na barabara ya Kalobe yenye urefu wa kilometa 3.5 na kufanya jumla ya kilometa 12.3 kwa kiwango cha lami.

Diwani Kata ya Mbalizi Road, Adam Simbaya amemtaka mkandarasi aliyepewa zabuni ya ujenzi wa mradi huo kutekeleza kwa ubora ili kuepuka changamoto ya kujenga chini ya kiwango.

“Kuna baadhi ya barabara zinajengwa chini ya kiwango na kupelekea baada ya muda mfupi kuchakaa hilo tunatoa angalizo kupitia mradi huo mkubwa wa barabara za ndani.

Mkazi wa Sokomatola, Sikujua Aloyce ameishukuru Serikali kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya barabara za pembezoni kwani zitachangia kukua kwa shughuli za kiuchumi.