DC Mbeya: Wabadhirifu fedha za miradi wafichuliwe

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa akizungumza na wajumbe wa baraza la Jumuiya ya Umoja wa Vijana (Uvccm) Wilaya ya Mbeya mjini kwenye kikao cha kikanuni kilichofanyika katika Ukumbi wa Dk Tulia. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa, ameagiza uongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (Uvccm) Wilaya ya Mbeya mjini kuibua hoja zenye mashiko zitakazosaidia kufichua wabadhirifu wa fedha za umma.

Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa, ameagiza uongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (Uvccm) Wilaya ya Mbeya mjini kuibua hoja zenye mashiko zitakazosaidia kufichua wabadhirifu wa fedha za umma.

Malisa amesema leo Jumanne, June 7, 2023 wakati akifungua kikao cha Baraza la Kikanuni la umoja huo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Dk Tulia uliopo katika Ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya.

Amesema kuwa katika nyakati za kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa vijana ndani ya chama wanatakiwa kuanza kutembelea utekelezaji wa miradi ya Maendeleo inayoelekezwa na Serikali ya awamu ya sita kuanzia ngazi za mitaa na kata.

“Serikali na chama tunawategemea vijana sasa mnapaswa kuisaidia kufichua palipo toboka na kuvuja, ili kuwezesha kutatua changamoto hususan kwa vijana wa bodaboda na wafanyabishara wadogo (Machinga) jijini hapa,” amesema.

Malisa ameongeza kuwa wakati huu tunaelekea kwenye uchaguzi wa nafasi wa Serikali za mitaa tunahitaji vijana ndani ya chama kuanza kuifutilia miradi na kuielezea kwa wananchi na kwamba itakayotiliwa shaka basi watoe taarifa mapema.

Amesema ni wakati sasa wa kuibua hoja zenye mashiko, na changamoto zilizopo kwenye jamii yetu ambazo zitaleta tija na chachu kwa Serikali kuzitatua ikiwepo suala zima la uwezeshwaji kwa vijana wakiwepo machinga na bodaboda.

“Asilimia 90 ya vijana ni Bodaboda na Machinga sasa ni jukumu lenu vijana ndani ya chama kuisemea Serikali mambo inayofanya ikiwepo kusikiliza changamoto na kuzileta ili Serikali izitatue kwa wakati,” ameongeza.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya hiyo, Clemence Mwandemba amesema wanakila sababu ya kufuatilia miradi ya umma lengo likiwa ni kuisemea Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Tunashuhudia miradi mikubwa ambayo imeelekezwa mkoani hapa ikiwepo ujenzi wa barabara njia nne, mradi wa maji mto Kiwira na mingine mingi ambayo kwa namna moja ama nyingine inachochea maendeleo na ajira kwa vijana,” amesema.

Amesema uwepo wa miradi hiyo ni jitihada za Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson kuyasemea matatizo ya wananchi wake katika vikao vya bunge mjini Dodoma.

Aidha ameihakikishia Serikali vijana kuwa chachu ya kuibua changamoto za jamii, ubadhirifu wa fedha za miradi, sambamba na maandalizi ya kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Sabasaba, Ally Mbika amesema  utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi hususan sekta ya afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara imeleta neema kwa wanambeya na kuomba jamii kuendelea kuunga mkono .