Maduka 43 yateketea Tunduma

Muktasari:
Moto ulioanza kuteketeza maduka katika Soko la Manzese mjini Tunduma mkoani Songwe kuanzia alfajiri ya leo Jumanne Novemba 16, 2021 umedhibitiwa huku maduka 43 yakiteketea.
Tunduma. Moto ulioanza kuteketeza maduka katika Soko la Manzese mjini Tunduma mkoani Songwe kuanzia alfajiri ya leo Jumanne Novemba 16, 2021 umedhibitiwa huku maduka 43 yakiteketea.
Moto huo umedhibitiwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wananchi.
SOMA ZAIDI: Moto wateketeza soko Tunduma
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Janeth Magomi amesema moto huo umetekeza jengo lenye maduka 43 ambapo kati ya maduka hayo 10 hayakuwa na bidhaa.
Kamanda Janeth amesema kuwa chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na uchunguzi unaendele.
Mkuu wa Wilaya ya Momba, Fakii Lulandala amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa jitihada za kuudhibiti moto kwa kiasi kikubwa licha ya gari la zimamoto la Tunduma kutokuwepo eneo hilo kutokana na kuwepo kwenye matengenezo jijini Mbeya.
Amesema wamelazimika kutumia gari kutoka Vwawa Wilaya Mbozi kuzima moto huo.
Lulandala amesema soko la Manzese lina zaidi ya vyumba 700 lakini jeshi la zimamoto limedhibiti moto kutosambaa kwenye majengo mengine
Mkuu huyo wa Wilaya ameliagiza Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Tanesco kufanya uchunguzi hili kubaini chanzo cha moto huo huku akitoa rai kwa wananchi kuwa wapole.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Songwe, Joseph Kapange amesema baada ya kupata taarifa walijitahidi kuwahi ili kuweza kuzima moto usisambae kwenye majengo mengine.
Kapange amesema baada ya kuudhibiti moto huo watatoa taarifa kamili ya nini kilichosababisha.